REA YAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA WAJASIRIAMALI SONGWE

August 16, 2025
-Wahamasishwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye eneo hilo

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa wito kwa Wajasiriamali Nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia eneo la Nishati Safi ya Kupikia ili kujizalishia kipato sambamba na kuunga mkono Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kulinda afya na kuokoa mazingira.

Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali ametoa wito huo Mkwajuni Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe Agosti 16, 2025 katika Kongamano la Wajasiriamali Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe lililoratibiwa na Mtandao wa Kuinua Wanawake Kiuchumi Tanzania (TAWEN) na kuhusisha zaidi ya washiriki 350.

"Wajasiriamali wanayo nafasi kubwa ya kufaidika na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani katika Sekta ndogo ya Nishati Safi ya Kupikia," alibainisha Dkt. Sambali.

Alizitaja baadhi ya fursa kuwa ni pamoja na uwakala na uzalishaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia kama vile mkaa mbadala na majiko banifu.

Alisisitiza kuwa matumizi ya Nishati Safi ya kupikia ni muhimu katika kuepusha magonjwa yanayotokana na uvutaji wa hewa chafu inayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama.

Aliongeza kuwa matumizi ya Nishati Safi ya kupikia yanasaidia kuepusha athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi inayosababishwa na ongezeko la hewa chafu na ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWEN Nyanda za Juu Kusini, Oliva Hasukenye alisema wanaunga mkono Kampeni ya Nishati Safi ha Kupikia na wanaendelea kuhamasisha kupitia majukwaa mbalimbali.

"Sisi TAWEN tunaunga mkono kampeni hii ya Nishati Safi ya Kupikia kwani maisha ya kutumia nishati isiyo safi na salama tumeyaishi na madhara yake tunayaelewa na tumedhamiria kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kuelimisha jamii kuhusiana na madhara hayo," alisema Hasukenye.

Alisema Mjasiriamali ambaye anatumia Nishati Safi Kupikia hawezi kuwa sawa na yule ambaye anatumia nishati zisizosafi wala salama kuanzia katika kipato hadi usafi wa mazingira anayofanyia kazi.

Naye mshiriki wa kongamano Juma Ramadhani ambaye ni mjasiriamali kutoka Mkwajuni alipongeza elimu aliyopata ya Nishati Safi ya Kupikia na kuahidi kubadilisha mtindo wake wa maisha kwa kuanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia.

Ramadhani aliahidi kuwa balozi wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wajasiriamali ambao hawakupata fursa ya kushiriki na kwa jamii nzima kwa ujumla.

Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatumia njia mbalimbali kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »