DKT. BITEKO ATAKA WATUMISHI WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE KUWA MFANO WA MATUMIZI NISHATI SAFI YA KUPIKIA

August 22, 2025
-Lengo ni kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo

-Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yapaa kutoka asilimia 6 hadi 20.3

-Agawa majiko yanayotumia umeme kidogo kwa Watumishi wa Wizara ya Nishati na REA

- Apongeza REA kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka watumishi katika Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini ya wizara hiyo kuwa mfano katika matumizi ya Nishati Safi ya kupikia ili kuitekeleza kwa vitendo ajenda iliyoasisiswa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama kwa afya

Maelekezo hayo ameyatoa tarehe 22 Agosti 2025 jijini Dodoma wakati akigawa majiko yanayotumia umeme kidogo kwa watumishi wa Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo amewataka Watumishi hao wawe mabalozi katika kutekeleza ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia.

" Leo tunagawa majiko haya kwa kuwa nyinyi ndiyo wenye dhamana kuu ya kutekeleza Ajenda ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia hivyo wajibu wenu ni mabalozi wazuri kwa watu wanaowazunguka ili nao wahamasike kutumia nishati hii safi." Amesema Dkt. Biteko

Amesema kufuatia mwamko mkubwa unaoendelea sasa kwa wananchi kufahamu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia, kiwango cha watumiaji kimepanda kutoka asilimia 6 na kufikia asilimia 20.3 huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 80 ifikapo 2034.

Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa Idadi ya watu wanaoendelea kutumia nishati isiyo safi na salama ya kupikia bado ni kubwa duniani, barani Afrika na hapa Tanzania hivyo ni jukumu la watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuhakikisha watanzania wanapata elimu sahihi ili waweze kubadilika na kufikia lengo lililokusudiwa.

Akigawa majiko 220 kwa watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Biteko amepongeza Taasisi hiyo kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan katika maeneo ya vijijini ambapo kumeonekana kuwa bado changamoto ya kufikiwa na Nishati Safi ya Kupikia.

Pia ameipongeza REA kwa kuhakikisha Vijiji vyote 12,318 nchini vinafikiwa na umeme.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amemhakikisha Dkt. Biteko kuwa atakahikisha agizo alilolitoa linatekezwa na Taasisi zote anazozisimamia.

Amesema atahakikisha kwamba Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia yanafikia malengo yaliyokusudiwa.

Amewasisitiza watumishi kutumia Majiko hayo waliyopewa na si kuyahifadhi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »