NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu, kimebuni mashine ya kisasa ya kuuza vinywaji baridi inayojiendesha yenyewe bila kuhitaji uwepo wa mtu kwa ajili ya kutoa huduma kwa mteja.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhadhiri Mwandamizi wa UDOM, Bw. Hassan Kilabo, amesema mashine hiyo inalenga kurahisisha huduma kwa wateja huku ikipunguza gharama za uendeshaji wa biashara kwa kuondoa hitaji la wahudumu.
“Mara baada ya mmiliki kuweka bei na kuweka maelekezo ya matumizi, mashine hutoa huduma kikamilifu bila kuhitaji mtu. Imeunganishwa na mifumo mitatu ya malipo: kupitia sarafu, noti, na lipa namba,” amesema Bw. Kilabo.
Mashine hiyo ya kipekee, inayopatikana kwa oda maalum, inachukua takriban miezi miwili kuandaliwa na kugharimu shilingi milioni 14. Ubunifu huu umetajwa kuwa suluhisho la kisasa kwa wafanyabiashara wanaotaka kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za ajira.



EmoticonEmoticon