Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ametembelea eneo la ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo iliyopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, mnamo tarehe 2 Julai 2025 na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo. Ziara hiyo imelenga kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kampasi hiyo ikiwa ni ufadhili wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Prof. Nombo alipata fursa ya kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa majengo yanayojengwa katika eneo hilo, na kujionea kasi pamoja na viwango vya ubora vinavyotumika. Akiwa kwenye ukaguzi huo, Prof. Nombo alitoa pongezi kwa namna kazi inavyoendelea na akasisitiza kuwa Menejimenti ya Chuo inapaswa kuhakikisha usimamizi wa karibu ili kazi zikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, Prof. Nombo alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa kozi za amali katika kampasi hiyo, ambazo zitamjengea mwanafunzi uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Pia alieleza kuwa uwepo wa baadhi ya wajumbe wa Menejimenti katika ukaguzi huo ni jambo jema litakalosaidia usimamizi madhubuti na kuharakisha utekelezaji wa mradi kwa ufanisi zaidi.
Prof. Nombo amemtaka Mkandarasi kuzingatia ubora katika kila hatua ya ujenzi na kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa wakati ili wanafunzi waanze kudahiliwa ifikapo mwaka wa masomo ujao. Vilevile, Prof. Nombo alihimiza matumizi ya vijana waliomaliza mafunzo ya ufundi kupitia vyuo vya VETA, hasa wale wanaotoka mkoa wa Tanga, ili kuwapa fursa ya kuchangia katika ujenzi wa kampasi hiyo na kunufaika kiuchumi.
Pia alisisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa takwimu kuhusu namna jamii ya Kata ya Gombero imenufaika na uwepo wa mradi huu, hususani kwa upande wa ajira, huduma, na fursa nyingine za kiuchumi.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya elimu ya juu nchini, kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora, kwa wakati, na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi ambapo alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 57.5. Alifafanua kuwa hosteli za wanafunzi zimekamilika kwa asilimia 58, nyumba za watumishi kwa asilimia 68, jengo la taaluma kwa asilimia 57, bwalo la chakula kwa asilimia 56 na kituo cha afya kwa asilimia 58.
Alieleza kuwa licha ya changamoto za hapa na pale, mradi unaendelea kwa kasi nzuri kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya Chuo, Mkandarasi na wadau wengine wanaohusika katika utekelezaji na usimamizi wa mradi huo
Katika ziara hiyo, Prof. Nombo aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo pamoja na timu ya Mkandarasi wa Ujenzi kutoka kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Ltd.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo akikagua maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo kikuu mzumbe jijini Tanga na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa huo ambao umefikia asilimia 57.5. Katikati ni Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha na sehemu ya wajumbe wa menejimenti.
Msimamizi wa Mradi upande wa Mkandarasi (Dimetoclasa Real Hope Limited) Mhandisi John Bhoke akieleza kuhusu hali ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Carolyne Nombo. Ujenzi unaoendelea katika Kampasi hiyo ni pamoja na kumbi za mihadhara, Hosteli za wanafunzi, Kituo cha Afya, Nyumba za watumishi na Bwalo la Chakula.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Carolyne Nombo akikagua Mradi wa ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga. Ujenzi huo unafanya na Kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited na umefikia asilimia 57.5. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba.
EmoticonEmoticon