MRADI WA BOMBA LA GESI NTORYA–MADIMBA KUGHARIMU SHILINGI BILIONI 120

July 03, 2025
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba wa makubaliano na kampuni ya China ya CPP na CPTDC kwaajili ya ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Ntorya hadi Madimba mkoani Mtwara kwa kipindi cha miezi 12.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Julai 3, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Mussa Makame amesema bomba litakalojengwa litakuwa na uwezo wa kusafirisha gesi ya futi za ujazo milioni 140 kwa siku, kiwango ambacho kinauwezo kuzalisha umeme wa megawati 700.

Katika utekelezaji wa ujenzi wa bomba hilo, Makame amesema vijiji 11 vitapitiwa na mradi huo na tayari tathmini ya mazingira imefanyika pamoja malipo ya fidia kwa watakaopitiwa na mradi.

Amesema watatumia takribani Sh120 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Aidha Makame amesema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa Bomba, kazi itakayofanywa na TPDC na kazi ya uchimbaji wa visima itafanywa na Kampuni ya ARA Petroleum, kazi ambayo itakamilika kwa miezi 12.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CPP ya China Bai Zhengshuai amesema mradi huo wataukamilisha kwa wakati na watazingatia Sheria za nchi wakati wa ujenzi wa bomba hilo.

"Mradi huu tutautekeleza kwa wakati na tutafuta sheria za nchi,mradi huu kwetu tutaufanya kwa ufanisi ili kuendeleza ushirikiano wetu,"amesema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »