Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
BENKI ya NMB imetoa Jumla ya Sh170 milioni kama sehemu ya udhamini wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT). Kiasi hicho ni sehemu ya jumla ya fedha Sh1.4 bilioni zilizokwishakutolewa na benki hiyo kwa ajili ya ALAT katika kipindi cha miaka 9 tangu NMB ilipoanza kuwadhamini.
Mkutano huo unafanyika Jijini Dodoma kuanzia kesho Machi 11,2025 ambapo mgeni ramsi anatarajia kuwa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan.
Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali Alfred Shao, amekabidhi hundi kwa uongozi wa ALAT leo Machi 10,2025 huku akisisitiza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na chombo hicho kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Shao amesema ndani ya kipindi hicho wamepata ushirikiano wa kutosha kutoka ALAT na hivyo hawaoni shida ya kuendelea kuwadhamini na kwamba wanafanya hivyo kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
“Pamoja na kiasi hiki, itakumbukwa tulianza kutoa mchango wetu karibu miaka 9 iliyopita na hadi leo tutakuwa tumefikisha Jumla ya Sh1.4 bilioni, tunaamini mashirikiano haya tutayaendeleza,” amesema Shao.
Afisa huyo amesema fedha walizokabidhi kwa leo, Jumla ya Sh100 milioni zinatolewa kama fedha taslimu wakati Sh70 milioni zinatolewa kama vifaa na huduma zingine.
Hata hivyo amewakaribisha wajumbe wote wa ALAT kushirikiana na benki hiyo katika ibada ya futari itakayofanyika kesho Jumanne Machi 11,2025 ili wajumuike kwa pamoja na kupata muda wa kubadirishana mawazo huku akisisitiza kuwa, katika kipindi chote cha Mkutano huo NMB wataendelea kutoa huduma zao katika banda lao lililopo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center (JKCC).
Mwenyekiti wa ALAT Murshid Ngeze amesema yapo mengi ambayo chombo hicho kinajivunia baada ya kuanzisha ushirikiano na NMB lakini kikubwa ni jinsi Benki hiyo ilivyowarahisishia huduma kwa wananchi wao.
Ngeze amesema hawajawahi kukwama jambo lolote katika kuwahudumia wananchi kupitia Halmashauri huko vijijini baada ya NMB kufika karibu maeneo yote na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
“Asubuhi nilikuwa kwenye kipindi kimoja na TV furani (anaitaja) waliniuliza swali kwamba sisi ALAT tunanufaikaje kuwa karibu na NMB, nimewambia vitu vingi, lakini hatujawahi kukwama kwenye huduma zetu ndani ya Halmashauri yoyote iliyojiunga na mtandao wa NMB, hakika hawa ni ndugu zetu na zaidi ya ndugu,” amesema Ngeze.
Makamu Mwenyekiti wa ALAT Sima Constantine amesema hakuna kitu wala jambo linaloweza kuwazuia kuwa na ushirikiano na NMB kwani mara nyingi wamekuwa wakipata mafanikio makubwa ndani ya benki hiyo.
EmoticonEmoticon