VIONGOZI WATENDAJI WA SERIKALI ZA MITAA WILAYA YA SAME WAPEWA MAFUNZO MAALUMU

February 04, 2025

 

Ashrack Miraji 

 Katika kutambua umuhimu wa haki za binadamu na utawala bora, Viongozi na watendaji wa serikali za mitaa  wilaya ya Same wamepewa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo ili kuhakikisha wanaimarisha uwajibikaji, usawa na utawala wa sheria na haki katika jamii.

Akizungumza wakati wa ufungunzi wa mafunzo elimu ya Uraia na Utawala bora kwa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, Mkuu wa wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni amesema kuwa mafunzo haya yana umuhimu mkubwa katika uongozi na kuwasaidia watendaji kuelewa vyema misingi ya haki za binadamu na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kama watumishi wa Umma ni lazima tuyafahamu haya yote katika utekelezaji wa majukumu yetu kupitia maada hizi muhimu ambazo zinaenda kutukumbusha, niwaombe sana baada ya mafunzo haya tunatarajia kuona utekelezaji ili kutokukiuka taratibu, kanuni na miongozo katika utumishi wa Umma” amesema Mhe. Kasilda.

Naye Afisa Uchunguzi mkuu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Bi. Juliana Laurent amesema zipo changamoto zinazoathiri utawala bora na haki za binadamu ikiwa ni pamoja na umaskini, uelewa mdogo wa wananchi katika maswala ya haki za binadamu hasa linapokuja jambo la kimahakama pamoja na mila potofu.

“Zipo baadhi ya changamoto zinazoathiri utawala bora  katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo changamoto ya umaskini, mila potofu katika jamii pamoja na uelewa mdogo wa wananchi katika maswala ya haki za binadamu hivyo ni lazima tuhakikishe tunaondoa vikwazo hivyo kwa kulinda na kudumisha haki za binadamu” amesema Bi. Juliana.                           

Pia Wakili Prosper Kisinini ambaye ni mratibu wa mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala bora mkoa wa Kilimanjaro amewasisitiza watendaji hao wa serikali za mitaa kuwa na Usawa, uwazi, ustahimilivu na wasikivu katika kuwahudumia wananchi na kueleza kuwa serikali haitegemei kuona watendaji wanazozana na wananchi katika utekelezaji wa majukumu.

“Ni lazima viongozi kwenye maeneo yenu muwe na uwazi, usawa, ustahimilivu na wasikivu katika kuwahudumia wananchi, tunapaswa kuwashirikisha wananchi kwenye maeneo yetu kwa kila jambo ili waweze kusimama katika misingi ya utawala bora na demokrasia”

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria ambayo yanatolewa nchini kote yenye lengo la kuwajengea uwezo watendaji wa serikali za mitaaa katika kuimarisha utawala bora na haki za binadamu na kuleta ustawi kwa wananchi



 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »