UTENDAJI KAZI KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA TANESCO WAMKWAZA DKT.BITEKO

February 04, 2025


📌 *Amuagiza Mkurugenzi Mtendaji TANESCO kumchukulia hatua mtaalam aliyemfokea mteja*


📌 *Ataka Mpango Mahsusi wa Nishati uliosainiwa katika Mkutano wa Mission 300 kupewa kipaumbele*


📌 *PURA, REA, EWURA zang'ara tathmini ya utendaji kazi Taasisi chini ya Wizara ya Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kutoridhishwa kwake na Kituo cha Huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kusema huduma duni zinasababisha malalamiko kutoka kwa wateja.


Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati wa Kikao cha Tatu cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2024 ikiwa ni utaratibu aliouanzisha kwa lengo la wa kujipima katika kila baada ya miezi mitatu ili kuboresha utendaji wa kazi wa Wizara na Taasisi zake.


“Pamoja na kazi zote nzuri mnazozifanya lakini eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni utoaji wa huduma kwa wateja, juzi nilitembelea kituo hiki nikawaambia sifurahishwi na utendaji kazi wa kituo,  mimi nafahamu changamoto za kituo hiki si kwa kuota bali wananchi wananipa mrejesho pamoja na viongozi wanaonisimamia, hivi tumefanya kazi yote hii ya kuwa na umeme wa ziada, tunajenga laini za umeme, lakini mtu  mmoja ambaye kazi yake ni kumsikiliza mteja na kumpa majibu sahihi anatupaint wote vibaya tunaonekana hatufai, majibu yapo lakini wataalam wanageuka kuwa wababe kwa wateja, hii hakubaliki.” Amesema Dkt. Biteko


Dkt. Biteko ametolea mfano lalamiko la mwananchi la kupiga simu TANESCO kisha akapewa tiketi namba ya lalamiko lakini baada ya muda tiketi namba hiyo ilifutwa kwa madai kwamba lalamiko husika limeshashughulikiwa huku ikiwa sikweli, hata hivyo baada ya mteja kuuliza kwa nini lalamiko lake limefutwa aliishia kufokewa.


Kutokana na hilo, Dkt.Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuchukua hatua kwa mtaalam aliyehusika na suala hilo na endapo TANESCO haitachukua hatua ifikapo ijumaa wiki hii, atachukua hatua huku akisisitiza kwamba heshima kwa wananchi lazima iwepo na Wataalam wa Kituo cha Huduma kwa wateja wanapaswa kuwapa majibu stahiki na ya staha wananchi na wawe ni sehemu ya kutatua shida za wananchi

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameziagiza Taasisi zote chini ya Wizara ya Nishati kuupa kipaumbele Mpango wa Mahsusi wa Nishati (Energy Compact) ambao ulisainiwa katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika tarehe 28 Januari 20225 ambao pamoja na masuala mengine ya nishati, umelenga kusambaza umeme kwa watanzania milioni 8.3 ifikapo 2030.

“Kila mmoja kwa nafasi yake ajipange atatekeleza vipi hii Energy Compact, fedha hizi mlizosikia zimetolewa na wadau wa maendeleo kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika zinahusu Bara lote la Afrika, hazitakuja Tanzania pekee hivyo lazima tujipange jinsi ya kupata hizi fedha ili kutekeleza miradi tuliyopanga kuifanya na tumheshimishe Rais, Dkt. Samia kwa kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji Mpango huu mahsusi ambao ni muhimu katika Sekta yetu ya Nishati.” Amesema Dkt. Biteko

Aidha, ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kwamba kazi ya usambazaji wa  nishati safi ya kupikia vijijini inaenda sambamba na  tathmini ya idadi ya watu wanaohama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi na Taasisi ijipange kuhakikisha kwamba ifikapo  mwaka 2030 asilimia 75 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.



Katika Kikao hicho cha Tathmini, Dkt. Biteko pamoja na Wizara ya Nishati walitoa zawadi kwa Taasisi zilizoshika nafasi za juu katika utendaji kazi ambazo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) iliyoshika nafasi ya kwanza, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulioshika nafasi ya Pili na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ulioshika nafasi ya Tatu. 

Pia ametoa zawadi kwa mikoa ya Kitanesco iliyofanya vizuri katika utendaji kazi ambayo ni Kilimanjaro (I), Kinondoni Kusini (II) na Kinondoni Kaskazini (III).

Kwa upande wake,, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameeleza kuwa  vikao vya tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake ambavyo muasisi wake ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati vimeleta matokeo chanya kwa kuleta mabadiliko ya utendaji kazi kwa Wizara na Taasisi zake.


Amepongeza Watendaji wa Wizara na Taasisi zake kwa kazi kubwa inayofanyika na inayoonekana katika macho ya wananchi ikiwemo uwepo wa nishati.


Mhe. Kapinga amewaasa watendaji na watumishi wa Wizara na Taasisi zake kufanya kazi kwa umoja na kwa kujitoa ili kuendelea kumheshimisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pamoja na Sekta ya Nishati kwa ujumla.


Taasisi zilizoshiriki Kikao cha Tatu cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Wizara na Taasisi zake ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja ( PBPA),  Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania

( TGDC).


Viongozi wa Wizara walioshiriki Mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio pamoja na Menejimenti ya Wizara.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »