KUPITIA KONGAMANO LA PETROLI LA EAC TUNATAKA NISHATI YA PETROLI IWE INJINI YA MAENDELEO - DKT.MATARAGIO

February 26, 2025



📌 *Tanzania kuchimba visima vya utafutaji Mafuta Eyasi Wembere*


📌 *CNG kufika hadi kwenye mikoa ambayo haijafikiwa na Bomba la Gesi*



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt.James Mataragio amesema Kongamano na Maonesho ya Petroli  ya Afrika Mashariki ( EAPCE'25 ) ambayo yatafanyika Machi 5 hadi 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam yanalenga kuhakikisha kuwa nishati ya petroli inakuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwenye Jumuiya ya Afrika.Mashariki.


Amesema hayo tarehe 26 Februari 2025 jijini Dar es Salaam katika Kipindi cha Jambo Tanzania kinachoendeshwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ikiwa ni muendelezo wa programu za kutoa elimu kwa umma kuhusu Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Machi 5-7 mwaka huu.


Amesema Tanzania ina rasilimali kubwa ya gesi ambayo iligunduliwa mwaka 1974 Songosongo iliyoanza kuzalishwa mwaka 2004  ambayo inatumika kwenye viwanda, magari, majumbani na kwa kiasi kikubwa inatumika kuzalisha umeme.



Ameeleza kuwa,  hivi karibuni shughuli za utafutaji mafuta zimeanza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Bonde la Eyasi Wembere ambapo Serikali inatarajiwa kuanza kuchimba visima vya utafutaji mafuta huku dalili zikionesha kuwa eneo hilo lina rasilimali husika.


Amesema kupitia EAPCE' 25 nchi zitabadilishana uzoefu katika masuala ya utafutaji wa mafuta huku Tanzania tayari ikiwa imeanza kubadilisha uzoefu na Uganda  hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo tayari imeshagundua rasilimali husika.



Kuhusu utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia kupitia mradi wa kusambaza gesi majumbani unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC)  amesema kuwa, mradi huo ni endelevu  na mikoa iliyo pembezoni mwa mkuza wa bomba la gesi kutoka Mtwara imeendelea kusambaziwa nishati hiyo.


 Ameeleza kuwa, Serikali pia inatilia mkazo ujenzi wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG)  ambayo itasafirishwa  kwenye mikoa ambayo bado haijafikiwa na bomba la gesi. Amesema ujenzi wa vituo hivyo unahusisha sekta binafsi.


Dkt.Mataragio ameeleza kuwa mwaka huu vitazinduliwa vituo 6 vya CNG ambapo mwezi ujao kitazinduliwa kituo kikubwa cha CNG katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.


Kuhusu Mkutano wa EAPCE' 2025 amesema umekuja wakati muafaka kwani unaleta wadau wote wa nishati ya petroli kutoka Afrika Mashariki na nchi nyinginezo ambao utatumika pia kama sehemu ya kujadili upatikanaji wa nishati ya kutosha ili kufikia malengo ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Misheni 300 ambao uliazimia kufikisha umeme kwa waafrika milioni 300 ifikapo 2030 .



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji TPDC, Derrick Moshi amesema kuwa Mkutano wa EAPCE utajumuisha  makundi mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara na  wawekezaji kwenye Sekta ya Mafuta, taasisi za kifedha, Wakandarasi wanaojihusisha na Sekta ya Mafuta, Watendaji kutoka Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Watafiti.


Amesema Mkutano utafungua fursa nyingi katika Sekta ya Nishati pamoja na sekta nyinginezo.


Ameongeza kuwa Mkutano huo utatumika kunadi vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu hivyo.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »