KITUO CHA KUPOZA UMEME CHA UHURU WILAYANI URAMBO KIMEKAMILIKA-MHE KAPINGA

February 07, 2025


*📌 Kinalenga kuboresha hali ya upatikanaji umeme Urambo na maeneo mengine*


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru kilichopo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora umekamilika.


Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Februari 07 2025 bungeni jijini Dodoma  wakati akijibu swali la la Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta aliyetaka kufahamu Serikali itakamilisha lini kituo hicho cha kupoza umeme na lini kitaanza kufanya kazi.


"Mhe. Spika ujenzi wa kituo cha kupoza umeme umeshakamilika, hivi sasa kazi inayoendelea ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme,  ikikamilika kituo hicho kitaanza kufanya kazi." Amesema Mhe. Kapinga


Akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu, Mhe. Ally Mhata aliyetaka kufahamu lini Serikali itashusha bei ya kuunganisha umeme katika Kata za Mangaka  na Kilimanihewa kama maombi yalivyowasilishwa Wizarani, Mhe. Kapinga  amesema kutokana na hali halisi ilivyo nchini, kuna maeneo ya vijiji na Vijiji Miji ambapo maeneo ya vijiji yanaunganishwa na umeme kwa gharama ya shilingi 27,000.


Ameongeza kuwa, maeneo yenye sura ya Vijiji-Miji yanaunganishwa kwa gharama ya shilingi 320,960 hivyo  kwa maeneo ya Kata ya Mangaka na Kilimahewa yenye sura ya Vijiji Miji yana unganishwa umeme kwa gharama ya shilingi 320,960.


Ameongeza kuwa,  Serikali inaendelea kuangalia kama kuna uwezekano wa kufanya maboresho ya gharama kutokana na tathmini iliyofanyika.


Kuhusu Vitongoji 105 ambavyo havijapata umeme Wilaya ya Nanyumbu, Mhe. Kapinga amesema hivi sasa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji ikiwemo Vitongoji 15 kwa Mbunge na kwa mwaka ujao wa fedha vitaongezwa Vitongoji vingine 38 ili kupunguza idadi ya vitongoji hivyo 105.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »