DKT.BITEKO AITAKA EWURA KUFANYA KAZI BILA KUYUMBISHWA,KUPINDISHWA

February 17, 2025



📌 *Vibali vituo vipya CNG vyatolewa, gharama za leseni zapunguzwa*


📌 *Morogoro, Makambako, Mbeya kutumika kushusha mafuta kutumia bomba la mafuta*


📌 *Afungua Baraza la Wafanyakazi EWURA*


📌 *Asisitiza mazingira mazuri, mafunzo kwa Watumishi*


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha kunakuwa na uendelevu wa  upatikanaji wa mafuta kwa wakati wote kwa gharama halisi, kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria na kutatua  malalamiko ya wateja kwa haraka ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania.


“Nawahakikishia kuwa wakati wote Serikali itaendelea kuwapa kila aina ya ushirikiano ili muweze kuwahudumia Watanzania, Serikali yoyote inapata heshima ikiwa inawahudumia wananchi ambao wana umeme na mafuta wakati wote hivyo, fanyeni kazi kwa kufuata sheria ili muwe salama, msikubali kuingiliwa na kupindisha misingi ya kazi.”Amesema Dkt. Biteko



Amesema hayo leo Februari 17, 2025 jijini Tanga wakati akifungua Kikao cha Nne cha Baraza la Pili la EWURA.


Dkt. Biteko ameipongeza EWURA kwa kutekeleza maagizo yake aliyoyatoa wakati wa kikao cha Baraza kilichofanyika mwezi Novemba 2024 ikiwemo kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko ya wateja, kuondoa urasimu katika utoaji wa vibali vya ujenzi wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari ( CNG), kupunguza gharama ujenzi wa vituo vya CNG,  kulegeza masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.



Kutokana na maagizo hayo ya Dkt. Biteko, kati ya Novemba 2024 na Januari 2025 EWURA imetoa vibali vya ujenzi wa vituo vinane vya CNG  huku wawekezaji 50 wakionesha nia ya kujenga vituo vingine.


Aidha, EWURA imeshusha gharama za leseni na vibali vya ujenzi vituo vya CNG  na gharama za maombi ya vibali zimepunguzwa  kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000 na gharama za maombi ya leseni zimeshushwa kutoka 1,000,000 hadi 100,000.



Dkt. Biteko pia ametoa  maagizo mbalimbali kwa uongozi wa EWURA ikiwemo kusimamia malipo na stahiki zote za kifedha za watumishi,  kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuwa  na vifaa na vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na muda, teknolojia na mahitaji yaliyopo kwa Taasisi na watumishi.


Maagizo mengine aliyoyatoa ni kuwaendeleza watumishi kitaaluma kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu, mfupi na wa kati katika fani mbalimbali ili kuisaidia  Taasisi na watumishi kuendana na mabadiliko na maendeleo ya Teknolojia yanayotokea ulimwenguni. Pamoja na kuboresha uhusiano kati ya uongozi na watumishi kwa kuanzisha mijadala ya wazi kuhusu maendelo na mipango ya baadaye ya Taasisi. 



“ Pia ni muhimu kutambua na kuthamini kazi nzuri za watumishi, vitu kama vyeti, barua za pongezi na  tuzo za ufanisi husaidia kuwafanya watumishi watambue kwamba wanathaminiwa na hivyo kuendelea kuongeza bidii." Amesema Dkt. Biteko



Vilevile, amesisitiza suala la motisha kwa wafanyakazi na kuanzisha utamaduni wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo ndani ya taasisi  na kwa kushirikiana na Taasisi nyingine.


Katika kikao hicho ambacho kitajadili bajeti ijayo ya mwaka 2025/26 na utekelezaji wa bajeti ya 2024/2025, Dkt. Biteko amewahimiza wajumbe kujadili utekelezaji wa malengo ya taasisi

 kwa kuzingatia ajenda ya Taifa katika masuala ya Nishati hususani matumizi ya nishati safi ya kupikia na upatikanaji wa maji kwa gharama inayostahili kwa wananchi wote.


“Naamini mtafanya tathmini kutoka katika Bajeti iliyopita na kuona ni nini tufanye ili kukidhi mahitaji ya Watanzania." Amesema Dkt. Biteko.


Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amesema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipatia nchi heshima kubwa kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kwa ajili ya kufadhili miradi hiyo.



Ameendelea  “ EWURA mnatakiwa kubeba ajenda hii ya nishati safi kwa kuelimisha umma kuhusu manufaa yake,  pamoja na nishati safi ya kupikia tunataka kuongeza bomba la kusafirisha mafuta na kuongeza matenki ya kushusha mafuta maeneo mbalimbali ikiwemo Morogoro na Makambako ili tuweze kuondoa changamoto ya magari yote kuja kujaza mafuta Dar es Salaam.”


Kwa  upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt.Batilda Buriani amesema kuwa EWURA imeendelea kusimamia ipasavyo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kuhakikisha kunakuwa na ushiriki kamilifu wa wazawa na maslahi mengine ya nchi.


Ameipongeza Ewura kwa kusimamia mwenendo mzima wa upatikanaji wa mafuta na hivyo kuwezesha mkoa huo kuwa na nishati ya mafuta ya kutosha.


Kuhusu umeme vijijini, amesema kuwa vijiji vyote 763 mkoani Tanga vina umeme huku kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 4,596 ikiendelea.


Akizungumzia utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia, Dkt.Buriani amesema Mkoa wa Tanga unaendelea na uhamasishaji wa matumizi ya nishati hiyo, ambapo taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 zipatazo 1493 zipo kwenye mchakato wa kuhama kutoka kwenye matumizi ya kuni kwenda kwenye gesi  huku Jeshi la Magereza likifanya vizuri zaidi kwa Magereza yake kuanza kutumia nishati safi.


Amesema mpaka sasa Tanga tayari imepokea mitungj ya gesi ipatayo 21,000 ambayo itatolewa kwa wananchi kwa  bei ya ruzuku kwa punguzo la asilimia 50 na kwamba mitungi hiyo itaendelea kutolewa kadri inavyopatikana lengo likiwa ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. 



Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza EWURA kwa kutekeleza maagizo mbalimbali yanayotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ikiwemo la kuhakikisha kunakuwa na vituo vingi vya kujazia gesi kwenye magari (CNG)  ambapo kuanzia mwezi Novemba hadi sasa tayari wametoa vibali nane vya ujenzi wa vituo vipya vya CNG huku wawekezaji wakiendelea kujitokeza.


Aidha, ameipongeza EWURA kwa kuhamasisha suala la Nishati Safi ya Kupikia kwa kutoa elimu kwa wananchi na pia kuwezesha baadhi ya makundi ya wananchi kwa mitungi ya gesi ikiwemo vituo vinavyotoa malezi kwa wazee na shule.


Ameongeza kuwa, Ewura pia imefanya kazi kubwa kwenye usimamizi wa mradi wa EACOP kwa kuhakikisha maslahi ya nchi yanazingatiwa pamoja na ushiriki wa wazawa ambapo amesema mradi huo umefikia asilimia 55.


Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt.James Andilile alisema Taasisi hiyo imetekeleza ipasavyo maagizo mbalimbali yaliyotolewa na  Dkt.Biteko k  wakati wa kikao cha Baraza hilo mwezi Novemba 2024 ikiwemo la kushughulikia kwa haraka malalamiko ya wateja yanayowasilishwa EWURA ambapo  amesema kuwa kwa kupitia Mkataba wa Huduma kwa Wateja wa Ewura inashughulia malalamiko kwa haraka.


Kuhusu agizo alilolitoa Dkt. Biteko la EWURA kuhamasisha uwekezaji kwenye vituo vya kujazia gesi kwenye magari ( CNG) ili kuweza kuwa  na vituo vingi,  amesema agizo hilo limeendelea kutekelezwa ambapo kati ya mwezi Novemba 2024 na Januari 2025 tayari EWURA imetoa vibali vya ujenzi wa vituo 8 huku wawekezaji 50 wakionesha nia ya kuwekeza.


Dkt. Andilile amesema Ewura inaendelea  kuhamasisha uwekezaji wa ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini  kwa kushirikiana na REA na kwa vituo vya CNG  Ewura imelegeza masharti ya uwekezaji wa vituo  ambapo maombi ya vibali yamepunguzwa gharama kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000 na maombi ya leseni yamepunguzwa kutoka 1,000,000 hadi 100,000.


Aidha, kuhusu agizo alilotoa Dkt.Biteko kwa Ewura la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya Kupikia, Dkt. Andilile amesema kuwa taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo ya kuwaambia wananchi kuwa kuwa 

Gesi ya kupikia ni Salama.

Akizungumzia bajeti ya mwaka 2025/2026 itakayojadiliwa kwenye mkutano huo, Dkt.Andilile amesema kuwa Ewura imepanga kuwa na mifumo ya teknolojia itakayorahisisha kazi za udhibiti ili zifanyike kisasa na kwa ufanisi 


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »