Na Happiness Shayo-Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki (UNODC ROEA), imejipanga kushirikiana zaidi katika kupambana na uhalifu unaoathiri mazingira yanayolinda bayoanuwai.
Hayo yamejiri leo Februari 17,2025 katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na Mwakilishi wa Kanda wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki (UNODC ROEA), Bi.Ashita Mittal, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Chana amesema kupitia kikao hicho Wizara ya Maliasili na Utalii na UNODC wamepata fursa ya kuangalia jinsi UNODC inavyounga mkono juhudi za Tanzania za kukabiliana na uhalifu unaoathiri mazingira, kuangazia miradi inayoendelea, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa wanyamapori, uhalifu wa uvuvi na juhudi za usalama wa baharini.
Pia, Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zangu za dhati kwa UNODC kwa msaada wa kifedha na kiufundi unaotolewa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kupambana na uhalifu wa kimataifa unaojumuisha lakini sio tu Biashara Haramu ya Wanyamapori (IWT) kupitia Kitengo cha Pamoja cha Kudhibiti Bandari - JPCU.
“Biashara Haramu ya Wanyamapori sio tu inaleta vitisho vya usalama kwa urithi wetu wa asili lakini pia inadhoofisha juhudi za uhifadhi wa bioanuwai miongoni mwa nchi wanachama ambapo umeathiri vibaya uchumi wetu na kuzidisha uhalifu mwingine wa kupangwa kama vile utakatishaji fedha, ufisadi, dawa za kulevya na biashara haramu ya silaha kutaja machache.
Kwa upande wake Bi.Ashita Mittal ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa mafunzo ya kujengea uwezo kuhusu namna ya kukabiliana na Biashara Haramu ya Wanyamapori huku akisisitiza kuwa ni muhimu kushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto hiyo.
“Hatuhitaji pesa nyingi lakini tunahitaji kuangalia namna ya kuwajengea uwezo watu wetu na kushirikiana na jamii katika kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori lakini tunahitaji wafadhili wa kutusaidia” amesema Bi. Mittal.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
EmoticonEmoticon