Na Ashrack Miraji
Kufuatia taarifa za ujauzito kwa wanafunzi wanne wa shule tofauti za msingi na sekondari katika kata za Kalemawe na Bendera, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ameagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mhe. Kasilda ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, pamoja na kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto shule, Amehimiza umuhimu wa kuwasaidia na kuwapeleka shule watoto wanaoanza chekechea, darasa la kwanza, na waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza ili kufanikisha ndoto zao.
Akiongea kwa uchungu, Mhe. Kasilda amesisitiza kuwa vitendo vya kuwapa mimba wanafunzi vinaharibu ndoto za watoto wa kike na juhudi za serikali ya awamu ya sita, ambayo imejikita kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wote, hasa wa kike.
"Mazingira rafiki ya elimu yanayoboreshwa na serikali yetu ya awamu ya sita yanahitaji msaada wa jamii. Vitendo kama hivi havikubaliki, vinaharibu maisha ya watoto wetu na kukiuka maadili yetu. Wahusika wote watawajibishwa kwa mujibu wa sheria," amesema kwa msisitizo.
Mhe. Kasilda pia amewataka wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanalelewa kwa maadili mema na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kuathiri maendeleo yao ya kielimu na maisha yao kwa ujumla. Ameagiza pia kukamatwa kwa wazazi wanaowaficha wanaume waliowapa mimba wanafunzi, akiwataja wazazi hao kuwa washiriki wa uhalifu kwa kuficha wabakaji.
"Hata wazazi walioshirikiana na wanaume waliowapa mimba wanafunzi kwa kupokea kitu kidogo nao hawatapona. Nimeagiza nao watafutwe na washitakiwe kwa kosa la kuficha wabakaji," ameongeza Mhe. Kasilda.
Wananchi walioshiriki mkutano huo walionesha kuridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na Mhe. Kasilda, huku wakiahidi kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa za wahusika wa ukatili dhidi ya wanafunzi.
Kwa upande wao, baadhi ya walimu wakuu wa shule hizo wameeleza kuwa changamoto kubwa ni ushirikiano mdogo kutoka kwa wazazi wa wahanga, ambao mara nyingi huficha ukweli na kuweka vikwazo katika upatikanaji wa ushahidi wa kisheria. Walitoa wito kwa wazazi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.
EmoticonEmoticon