WATENDAJI WA UCHAGUZI MIKOA YA ARUSHA, KILIMANJARO NA DODOMA WAPATIWA MAFUNZO YA UBORESHAJI

November 30, 2024

Na Waandishi wetu, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma

Watendaji wa uchaguzi kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dodoma leo tarehe 30 Novemba, 2024 wamepatiwa mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa zoezi la uboreshaji wa daftari hilo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, na Halmashauri za Wilaya ya Kondoa, Kondoa Mji na Chemba. Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba, 2024.

Akifungua mafunzo hayo jijini Arusha, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa watendaji hao kwa sababu ujuzi na elimu watakayopata itawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kufanikisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea umahiri watendaji wetu ili waweze kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata, ambao nao watatoa mafunzo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi, ambao ndio watakaohusika moja kwa moja na uandikishaji wa wapiga kura katika vituo,” amesema Jaji Mwambegele.

Pia, Jaji Mwambegele amesisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa watendaji waliowahi kushiriki katika mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ili kusaidia wenzao ambao hawajawahi kushiriki katika zoezi kama hili, na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Katika mkoa wa Kilimanjaro, mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa yalifunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Mbarouk Salim Mbarouk (Mstaafu). Akizungumza katika ufunguzi, Jaji Mbarouk amesisitiza kuwa mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikishaji wapiga kura, lakini ameonya kuwa hawataruhusiwa kuingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu.

“Kwa madhumuni ya kuleta uwazi, mawakala wa vyama vya siasa watasaidia kutambua waombaji wapiga kura katika maeneo yao, jambo litakalosaidia kupunguza vurugu zisizohitajika,” amesema Jaji Mbarouk. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa watendaji wa uchaguzi kutoa ushirikiano kwa mawakala hao na kuhakikisha maelekezo ya Tume yanafuatwa ipasavyo.

Vilevile, mafunzo hayo yalifanyika mkoani Dodoma, ambapo Mjumbe wa Tume na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari, alifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Jaji Asina amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa vifaa vya uandikishaji, akisema kuwa kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu.

“Vifaa vya uandikishaji vimenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo ni lazima tuvisimamie kwa umakini na kuhakikisha vinatumika ipasavyo katika maeneo yote ya uandikishaji,” amesema Jaji Asina.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na maafisa waandikishaji, maafisa TEHAMA, pamoja na maafisa ugavi kutoka halmashauri mbalimbali za mikoa hiyo. Washiriki walipata ujuzi wa jinsi ya kutumia mfumo wa Voters Registration System (VRS) pamoja na vifaa vya kisasa vitakavyotumika katika vituo vya kuandikishia wapiga kura. Vilevile, walifundishwa namna ya kukabiliana na changamoto za kiufundi zinazoweza kutokea wakati wa zoezi la uandikishaji.


Mroki Mroki
Online Reporter/Blogger
Mob: +255 755 373999
Email: mrokim@gmail.com.
Blog: https://mrokim.blogspot.com/
DODOMA, TANZANIA


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »