Na Pamela Mollel,Arusha
Wananchi wametakiwa kuepuka vyakula vyenye mafuta,sukari na chumvi kwa wingi ili kupunguza hatari ya kupata changamoto ya utapiamlo wa lishe ya kuzidi pamoja na magonjwa yasiyoambukiza katika jamii kama vile sukari,shinikizo la juu la damu,kiharusi na ugonjwa wa Figo
Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya Mh.Jenista Mhagama tarehe 30 Octoba 2024 jijini Arusha ikiwa ni siku ya maadhimisho ya lishe kitaifa
Waziri Mhagama anasema Tanzania huadhimisha siku hii kila mwaka ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu manufaa ya lishe bora
Pia amewataka Watanzania kuhakikisha wanakula mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali ikiwemo ulaji wa matunda,mbogamboga na vyakula vya asili ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza
"Wananchi chukueni hatua ya makusudi kwa kuwa makini kufanya uamuzi sahihi kila siku kuhusiana na ubora wa vyakula wanavyokula au kuwalisha watoto uwe ni mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali pamoja na virutubisho"anasema Waziri Mhagama
Aidha alitaja utapiamlo unaoikabili jamii kuwa ni Utapiamlo wa Lishe pungufu ikiwemo udumavu,ukondefu,uzito pungufu hususani kwa watoto,Utapiamlo wa upungufu wa vitamini na madini mwilini yaani njaa iliyojificha ikiwemo upungufu wa damu pamoja na Utapiamlo wa lishe ya kuzidi unaoambatana na uzito uliozidi au kiribatumbo pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kama sukari,magonjwa ya moyo na shinikizo la damu
"Ndugu zangu Watanzania Utapiamlo hudhoofisha makuzi ya watoto kimwili na kiakili,huathiri ubunifu na uwezo wa kufanya maamuzi wakati wa utu uzima pamoja na kupunguza tija na uzalishaji mali"Anasema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama aliwataka wataalamu wa afya na lishe katika ngazi zote kuhakikisha wanatoa elimu ikiwemo uhamasishaji jamii kuhusu ulaji unaofaa na matumizi ya vyakula vilivyongezewa virutubisho kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo vijijini
Kwa mwaka huu kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa "Mchongo ni Afya yako Zingatia unachokula".
EmoticonEmoticon