*MwanaFA ataka wananchi Muheza wachague wagombea wanaotokana na CCM Ili kazi ya kuleta maendeleo iwe rahis*
* Asema mapenzi ya vyama yasiyafanywe ushabiki wa Simba na Yanga
* Awakumbusha kwamba tangu Muheza ianzishwe 1974 haijawahi kupata miradi na fedha kama miaka minne ya Rais Samia.
* Asema ilani ya mwaka 2015-2020 wilaya ilijenga vyumba 20 tu vya madarasa
* Asema Rais Dkt Samia ametoa fedha maeneo mengi Ili kuhakikisha anaondoa kero za wananchi
* Asema CCM tangu ianzishwe 1977 inaminiwa kutokana na dhamira yake ya kuwatumikia wananchi
Muheza Novemba 25
MBUNGE wa Muheza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo mhe Hamisi Mwinjuma almaarufu MwanaFA, amewataka wananchi wilayani Muheza Novemba 27 kuwachagua wagombea wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi CCM Ili kazi ya kuleta maendeleo iwe rahisi.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara ulifanyika tarafa ya Bwembera, MwanaFA alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa CCM imekuwa ikichaguliwa kwasababu ndiyo yenye dhamira ya dhati ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Amewataka wananchi waendelee kukiamini katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Jumatano Novemba 27 kwa kuwachagua wagombea wa Chama hicho.
Alisema kamwe wasifanye mambo ya vyama kama ushabiki wa timu za mpira za Simba na Yanga kwakuwa uchaguzi ni maisha ya watu na viongozi katika kuleta maendeleo.
Aliwakumbusha wananchi wa Muheza kwamba tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo mwaka 1974 hakuna wakati wowote ule ambao serikali imeweza kugharamia miradi pamoja na kuleta fedha za maendeleo kama utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2024.
Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa miaka minne ameweza kuleta fedha nyingi ambazo zimeweza kugharamia miradi ya Elimu, afya, barabara, umeme pamoja na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.
Alisema wakati akiingia kuwa mwakilishi wa Jimbo la Muheza mwaka 2020 Muheza ilikuwa Haina shule za sekondari katika kata 13 na hadi sasa zimebaki kata mbili tu ambazo hadi kufikia 2025 kata hizo zitakuwa zimejenga shule hizo.
Alitoa mfano kwamba Kwa miaka minne tangu Rais Dkt Samia aingie madarakani, katika elimu waliweza kujenga vyumba 211 vya madarasa ya shule ya msingi na wakajenga vyumba zaidi ya 100 vya shule ya sekondari tofauti na utekelezaji wa ilani ya mwaka 2015-2020 ambapo kwa miaka mitano ilani ya uchaguzi ilitekeleza ujenzi wa vyumba 20 tu vya madarasa ya shule za msingi.
Kwa upande wa afya alisema kulikuwa na kituo cha afya kimoja cha Mkuzi, lakini sasa wamepewa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1.1 kujenga vituo viwili ambapo kimoja tayari kimejengwa kata ya Kwafungo kwa gharama ya shilingi milioni 500 na kimoja kitajengwa Kijiji cha Mgambo kata ya Misalai ambapo hadi sasa Wana kiasi cha shilingi milioni 649 lakini pia wameweza kupata hati umiliki kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Ili kukamilisha kituo cha afya Ubwari kilichopo mjini Muheza.
"Ndugu zangu wa Muheza Novemba 27 nendeni mkapige kura mkiwa kifua mbele kama mmepigwa ngumi za mgongo, mwende kuwachagua wagombea wa CCM kwasababu kazi imefanyika kwa kiwango kikubwa,"alisema MwanaFA.
"Mheshimiwa Rais anadhamira njema kabisa na Watanzania na anatoa fedha hizi kuturahisishia maisha sisi na wananchi wenzetu kuwe na maisha ya uhakika, maisha ya leo yawe rahisi kuliko jana na ya jana yawe bora zaidi kuliko ya kesho," alisema MwanaFA na kuongeza kusema kwamba,
"Kura mtakazopiga ni kulipa shukrani na fadhila kwa Mheshimiwa Rais wetu ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa miaka hii minene, hakika Rais ameing'arisha CCM na kutufanya tutembee kifua mbele kutokana na miradi tuliyoitekeleza kwenye ilani yetu ya uchaguzi,".
Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Katibu wa UVCCM mkoa wa Tanga Tedy Makiyao ambaye aliwaeleza wananchi kwamba sumu haijaribiwi Kwa kuonja hivyo wananchi wa Muheza wanayo sababu ya kuwachagua wagombea wa CCM ambayo ina utaratibu mzuri wa uongozi kuanzia ngazi ya Balozi, tawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa kuliko vyama vingine ambavyo havina hata ofisi za vyama vyao.
Alisema kuwa hakuna chama ambacho kinaweza kuwaletea maendeleo wananchi kama Chama Cha Mapinduzi ambacho kimejipambanua kuwaletea wananchi maendeleo hivyo wasifanye makosa.
Alisema vyama vingine vinekuja wakati wa uchaguzi lakini baada ya kumalizika uchaguzi hawaonekani hata kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao hivyo wananchi wasipoteze muda kuwachagua.
Alirejea kuwaeleza wananchi kwamba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameleta fedha nyingi nchini kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na madiwani wa kata na viti maalum wa Tarafa ya Bwembera ambao walipopata nafasi waliomba kura na kuelezea kwamba tarafa hiyo haitapoteza hata Kijiji na kitongoji chochote.
EmoticonEmoticon