Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Mdau wa maendeleo ya jamii na Wananchi kwa ujumla Bwana *Enock Koola* ambaye ni MCHUMI kitaaluma , amechangia sh 6,500 000 ( milioni sita na laki tano ) kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya ya ghorofa tatu ambalo linatarajiwa kuwa na Maktaba ya kisasa chumba Cha computer na ukumbi wa Mithiian
Enock Koola alitoa mchango huo kwenye hafla ya mahafali ya 28 ya kidato cha 4 yaliyofanyika shuleni hapo Agape seminary iliyopo kata ya Mamba wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo ndugu Enock Koola alikuwa mgeni rasmi .
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bwana Koola alisema fedha hizo zimetolewa na yeye pamoja na familia yake kwa lengo la kusaidia ujenzi wa maktaba hiyo, ambayo itawawezesha wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa weledi na kufikia malengo yao katika masomo. “Huu ni mchango wetu kwa wanafunzi wa Agape Seminary ili waweze kupata mazingira bora ya kujifunza. Niwaombe wazazi na walezi ambao watoto wao wanasoma hapa, wawe mfano kwa kuchangia maendeleo ya shule hii, hasa katika ujenzi wa maktaba hii,” alisema Bwana Koola .
Aidha, alizungumzia umuhimu wa kushiriki katika maendeleo ya elimu na kuwa sehemu ya mabadiliko chanya. “Elimu ni nguzo muhimu katika jamii na ndiyo ufunguo wa maisha. Nawaomba wazazi muwe sehemu ya mabadiliko, ili watoto wetu wapate elimu bora,” aliongeza.
Koola pia alipongeza juhudi za uongozi wa Shule ya Agape Seminary, akimshukuru Mkuu wa Shule na Viongozi wa dini wa Kanisa la Kiutheri ( KKKT) Dayosisi ya kaskazini kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea katika shule hiyo ikiwa ni pamoja na huduma za Afya
. Alisema kuwa shule hiyo inatoa mchango mkubwa kwa jamii kwa kuandaa vijana wenye elimu bora, na kwa kutoa ajira kwa walimu 32 na watumishi wengine 21 wa shule hiyo .
Koola alimalizia kwa kutoa ahadi kwa wanafunzi wa shule hiyo, akisema: “Nikiwa kama mdau wa maendeleo, mimi naahidi zawadi kwa wanafunzi wote watakaofaulu kwa division 1, ili kuwapongeza kwa juhudi zao.”
Katika hotuba yake, Koola alitoa miongozo muhimu kwa wahitimu wa shule hiyo;
Alisisitiza umuhimu wa kumcha Mungu, kuwa na umakini katika masomo, na kuepuka mienendo mibaya kama vile ulevi na uasherati.
. “Safari yenu imeanza rasmi, na ni muhimu kuongeza juhudi katika elimu yenu. Kuwa na hofu ya Mungu, jitunze kiroho na kimwili, na ujipe nafasi ya kufanikiwa,” alisema.
Aliongeza: “Kwa wanafunzi wa leo, ambaye atapata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha sita, ni muhimu kuwa na malengo na juhudi za kufikia ndoto zako. Kumbukeni kwamba elimu ni ufunguo wa mafanikio ya baadaye.”
Aidha Koola pia aliwashukuru wazazi, walezi na wachungaji walioshiriki katika mahafali hayo, na kuwataka washiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na kijamii. Aliwahimiza kushiriki kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakafanyika tarehe 27 November mwaka huu na kuwachagua viongozi wenye maadili mema, utashi na uwezo wa kuchochea maendeleo katika taifa letu.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Shule ya Agape Lutheran Seminary , Goodluck Lyimo alisisitiza umuhimu wa nidhamu kwa wanafunzi, akiwataka kuwa mfano mzuri katika jamii, hasa wanapokuwa nyumbani au wanapohitimu. “Nidhamu ni msingi wa mafanikio, na nashukuru kwa malezi bora mliyopata hapa shule,” alisisitiza
EmoticonEmoticon