📌 *Dkt Biteko Asema CCM Inaeleza Hoja, Wengine Maneno*
📌 *Dkt. Biteko Awataka Wananchi Kuchagua Viongozi Watakaotatua Shida Zao*
📌 *Mbogwe Yapiga Hatua Kimaendeleo*
📌 *Dkt. Biteko Asema Uchaguzi ni Mipango na CCM Imejipanga*
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi kuchagua wagombea wa CCM kwa kuwa wanaeleza hoja zake za kuondoa umasikini kwa wananchi huku vyama vingine vikitaja majina ya watu katika kampeni zake.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 22,2024 wakati akifungua Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Mbogwe zilizofanyika katika Uwanja wa Lulembela mkoani Geita.
“Nataka niwaombe wananchi wote twende tukachague viongozi wa CCM watakaoshughulika na shida zetu, CCM haitaki ushindi wa kubebwa tunataka ushindi halali na sababu ya ushindi halali tunayo kwa kuwa tumetekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi, tulihamasisha kwa wingi watu wetu kujiandikisha na tunaamini mtajitokeza kupiga kura Novemba 27, 2024,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema awali katika wilaya hiyo hakukuwa na shule ya sekondari, watoto walikuwa wakifaulu na hakukuwa na shule ya kuwapeleka, aidha kulikuwa na hospitali moja pekee. Kwa jitihada zilizofanywa na CCM sasa wilaya hiyo imekuwa na maendeleo kwa kupata miradi mbalimbali ikiwemo maji, barabara na umeme.
Amewahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM, ili kuwa na mnyororo wa uongozi kutoka chini hadi juu ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“ Ushindi ni mipango na CCM imejipanga na kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo wanaCCM tembeeni vifua mbele kwa kuwa Chama chenu kinatambua mahitaji yenu na kiko tayari kuyatekeleza,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga amesema kuwa CCM wataomba kura kistaarabu huku akiwahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM ifikapo Novemba 27, 2024.
Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Geita, Mhe. Rose Busiga amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali katika Mkoa wa Geita.
Ametaja baadhi ya miradi kuwa asilimia 100 ya vijiji vyote mkoani humo vina umeme na tayari Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya barabara, hospitali na shule.
Pia, amewahamasisha wananchi wa Bukombe kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kumchagua Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbogwe, Mathias Nyororo amesema kuwa katika vitongoji 335 vilivyopo katika wilaya yake vyama vingine vimeweka wagombea katika vitongoji 14 pekee, huku katika vijiji 87 wameweka wagombea 17 pekee.
*📌Awaomba kuchagua viongozi wenye maono*
*📌Atahadharisha dhidi ya viongozi wenye kuhubiri chuki na mgawanyiko*
*📌Wagombea waomba kuchaguliwa ifikapo Novemba 27*
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wasisahau safari iliyowafikisha katika nchi ya amani na maendeleo.
Dkt. Biteko amesema hayo Novemba 22, 2024 katika wakati akizungumza kwenye mkutano wa Kampeni za Serikali za Mitaa zilizofanyika katika Kata ya Lulembela, Wilaya ya Mbogwe, Geita.
Amewataka kujitokeza kuwachagua viongozi wenye maono na mwelekeo wa kuwaunganisha kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa. “ Tunachagua viongozi wenye uelewa wa matatizo na kujua namna ya kutatua matatizo ya wananchi” amesema Dkt. Biteko.
Wanambogwe mna haki ya kuchagua Chama chenye Sera zinazotekelezeka ambacho ni Chama Cha Mapinduzi na kuachana na wale wenye porojo na maneno maneno, kwa kuwa watu wangependa kupata maendeleo na wamechoshwa na maneno yanayolenga kuwagawa watu. “Wenzetu wanakuja kusema na kutukana watu” watu wa Mbogwe ikifika tarehe 27 jitokezeni kwenda kupiga kura” Hatuhitaji ushindi wa kubebwa, bali watu waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura.
“ Nimekuja kuwaomba mtuunge mkono kwa kupiga kura na kuchukua vijiji na vitongoji vyote” ameomba
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolaus Kasendamila amewashukuru wagombea waliopitishwa na kusema hadi sasa CCM imesimamisha wagombea bila kupingwa kwa asilimia 84 katika ngazi mbalimbali katika uchaguzi huu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mbogwe amesema wagombea 301 kati ya 335 CCM hawakupata upinzani na wagombea 70 kati ya 87 katika ngazi ya vijiji wamepita bila kupingwa.
Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga amewapongeza wanaCCM walioteuliwa kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
Amewaomba kuondokana na vitendo vyote vya uvunjifu wa maadili ikiwemo vitendo vya rushwa.
Amesema wilaya hiyo inapendeza kwa vile kuna karibu kila kitu, kama kuna mapungufu ni madogo. “ Wagombea mmeaminiwa na watu hivyo mtatakiwa kufanya kazi bila kumruhusu shetani,” amesema.
Hata hivyo, amewataka kushirikiana na kutowabagua wapinzani katika kuleta maendeleo ya watu ambao ndio lengo la CCM.
“ Mgeni rasmi umechangia kuleta maendeleo ya Wilaya ya Mbogwe nasi tunakuomba ukamwambie Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa tuko imara kutafuta maendeleo ya wananchi na tunamuunga mkono” amesisitiza.
MWISHO
Share this
EmoticonEmoticon