Na Mashaka Mhando,Korogwe,Oktoba 27
WANANCHI wa Kijiji cha Kwasunga kilichopo kata ya Magila-Gereza wilayani Korogwe, wameomba Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) mkoani Tanga, kuwawekea matuta katika Kijiji hicho Ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara eneo hilo na kusababisha vifo vya watoto wa shule.
Walitoa ombi hilo Oktoba 26 mbele ya ofisa wa polisi wa kata hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa polisi, Frank Tungaraza ambaye alifika kijiji hapo kushiriki ibada ya mazishi ya mwanafunzi Modesta Yusuph (7) aliyegongwa na gari na kufariki papo hapo akielekea shuleni.
Mzee John Augostino mmoja wa waombolezaji alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwekwa matuta kwasababu haipiti wiki mtoto mmoja anagongwa na kufariki kutokana na magari kupita kwa mwendokasi.
"Ndugu askari kwanza tunakushukuru kwa kufika katika mazishi haya, lakini tunawaomba mkae na Tanroads na muwaeleze sisi hapa Kwasunga tunahitaji matuta, watoto wetu wanagongwa na kufa Kila wiki wakivuka kwenda shule," alisema Augostino.
Askari huyo alipokea ombi hilo na kuwaeleza wananchi kwamba wachukue taadhari wanapovuka barabara na wawasaidie watoto, wazee na watu wenye mahitaji maalum wanapovuka barabara.
"Ndugu zangu poleni sana na huu msiba, lakini niwasihi mzingatie kanuni ya uvukaji barabara muwe makini na muwasaidie watoto, wazee na watu wenye ulemavu na muwaeleze uvukaji salama wa barabara," alisema na kuongeza,
"Malalamiko yenu nitayafikisha kwa Mkuu wangu wa polisi yaani OCD, kwani ni dhahiri alama pekee zilizopo hapa hazitoshi hasa kwa madereva ambao hawazingatii Sheria za usalama barabarani,".
Mkaguzi Msaidizi huyo wa polisi, pia aliwasihi wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi kwa kuvunja magari vioo au kuyachoma moto pindi yanaposababisha ajali kwani kwa kufanya hivyo ni makosa kisheria.
EmoticonEmoticon