WIZARA YA MALIASILI YAZIDI KUWA TISHIO KWENYE MICHEZO YA KIRAFIKI KUELEKEA SHIMIWI 2024

September 07, 2024

Na. Ashrack Miraji Matukio Daima - Dodoma
.
Wizara ya Maliasili na Utalii imeibuka mshindi kwenye michezo mitatu ya kirafiki iliyochezwa leo kwenye Viwanja vya Vijana vilivyopo Jijini Dodoma ikiwa ni maandalizi ya  kuelekea Mashindano ya SHIMIWI 2024 yanayotarajiwa kuanza  Septemba 18 mwaka huu  Mkoani Morogoro 

Katika michezo hiyo Wizara ya Maliasili imejinyakulia ushindi kwenye mchezo wa Kamba ( Ke) dhidi ya Timu ya Wizara ya Madini  kwa goli mbili kwa nunge, Kamba (Me) imeibuka  mshindi kwa goli mbili kwa moja dhidi ya Timu ya  Wizara ya Madini huku kwa upande wa Netboli (Ke) ikiichakaza Timu ya CRDB kwa goli 26 kwa 21

Akizungumza mara baada ya ushindi huo Mkurugenzi wa Idara  Sera na Mipango wa wizara hiyo  ambaye pia ni moja ya walezi wa Timu hiyo, Bw. Abdallah Mvungi ameipongeza Timu hiyo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuiletea Wizara ushindi huku akiitaka Timu hiyo kuongeza jitihada za kufanya  mazoezi ili kuiletea Wizara ushindi katika mashindano ya SHIMIWI 2024

"Wachezaji wetu, tunawapongeza sana kwa ushindi huu, Kila siku tunaona mabadiliko, mnacheza kwa moyo na ari kubwa sana, hongereni sana. Sisi tutaendelea kuwapa hamasa na kuwaunga mkono, endeleeni kupambana ili tutakapoenda kwenye mashindano tuiletee wizara Ushindi" Amesema Mvungi

Kwa upande wake Kocha wa Timu ya Kamba (Ke na  Me) wa Wizara hiyo , Bw. Abunu Issa  amewapongeza Wachezaji hao huku akiwasisitizia kuendelea kujitoa na kuhakikisha wanashinda michezo ya kirafiki itayofuata hapo kesho

Ameongeza kuwa, michezo ya kirafiki inayochezwa ni muhimu kwa Timu hizo kwani inawajengea ari ya kupambana lakini pia, inazisaidia timu hizo kujipima  kwa ajili ya maandalizi ya Mashindano ya SHIMIWI yanayotarajiwa kuanza  hivi karibuni

" Nanachoangalia katika michezo hii ya kirafiki ni hali ya wachezaji wetu  kama wanapokea kile ninachoelekeza na kufundisha, Hivyo, hii michezo ni kipimo tosha cha mimi kufahamu kama maelekezo yangu yanafuatwa  na kutekelezwa ipasavyo" Amesema Abunu

Kulekea Mashindano ya SHIMIWI 2024, Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajiwa kushiriki michezo kadhaa ya kujipima uwezo,  ambapo hapo kesho Wizara inatarajiwa kuchezo Mchezo wa Kirafiki kwenye mchezo wa Netboli pamoja na Kamba (Me) dhidi ya Timu ya  Wizara ya Utamduni sanaa na Michezo


 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »