MSIGWA AIPONGEZA TBS KWA KUHAMASISHA MICHEZO MAENEO YA KAZI

September 15, 2024

 



NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amezitaka taasisi mbalimbali za serikali kushiriki na kufanya mabonanza ya michezo ambapo itasaidia kuimarisha afya za wafanyakazi na kuleta manufaa kwa taifa kwa kuongeza idadi ya wachezaji na wawakilishi katika mashindano ya kimataifa.


Rai hiyo imetolewa Septemba14,2024 Jijini Dar es salaam alipokuwa katika Bonanza la michezo la watumishi lililoandaliwa na Shirika la viwango Tanzania (TBS).


Msigwa ameipongeza TBS kwa kuunga juhudi za Serikali ya awamu ya sita kwa kuhamasisha michezo maeneo ya kazi kwa kutengeneza bajeti na kuruhusu wafanya kazi kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya na kujenga mahusiano mazuri kazini jambo ambalo huoongeza ubunifu na ufanisi maeneo ya kazi.


Ameongeza kwa kuiasa Menejimenti ya TBS kutenga bajeti ya kujenga viwanja bora maeneo ya kazi ili kuwawekea wafanyakazi mazingira bora wakati wa kushiriki michezo mbali mbali.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi TBS Prof. Othman Chande amesema walianzisha Bonanza hilo miaka mitano iliyopita ambapo limelenga kuimarisha afya za wafanyakazi pamoja na kujenga umoja.


"Wachezaji wanacheza kama timu mbili tofauti lakini ni walewale wakishamaliza mchezo wanaenda pamoja inaongeza urafiki". Amesema


Aidha Prof.Chande ameeleza kuwa mashindano hayo ya mabonanza yatachangia kuwa na machaguo mengi ya wachezaji watakao wakilisha katika mashindano ya kimataifa.


Nae Mwenyekiti wa Michezo Shirika la viwango Tanzania (TBS) Nyabutwenza Methusela ameeleza faida za bonanza hilo ambapo amesema kuwa linasaidia watumishi kuondokana na changamoto ya afya ya akili kwa kujikita zaidi katika michezo ambayo inawaondolea msongo wa mawazo na kuongeza ufanisi wanaporudi kufanya kazi.


"Kupitia michezo afya ya akili na mwili inaboreshwa, wafanyakazi wanakuwa wachapakazi kwasababu wameboresha afya zao za akili pamoja na mwili". Nyabutwenza ameeleza.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »