Na Karama Kenyunko Michuzi TV
WADADISI na wasimamizi wa utafiti wa masuala ya kijamii na kiuchumi wametakiwa kuzingatia weledi na usiri mkubwa wakati wa ukusanyaji wa taarifa hizo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashim Abdallah amesema hatutawavumilia wale watakaotoa taarifa kabla hazijachakatwa na wakibainika watawachukulia hatua za kisheria.
Ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi hao zaidi ya 500 kutoka mikoa yote Tanzania Bara yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Dkt. Abdallah amewahimiza wenye viwanda na wafanyakazi watakaoombwa taarifa kutoa ushirikiano kwa ajili ya kupata takwimu sahihi kwa manufaa ya taifa.
"Kila mmoja anatakiwa ajue amebeba dhima ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, hivyo mzingatoe usiri na weledi wakati wa kukusanya taarifa," amesema Dkt Abdallah.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa NBS, Dkt. Amina Msengwa amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwanoa watafiti hao ili kwenda kufanya utafiti nchi nzima, kujua idadi kamili ya shughuli za kiuchumi kwenye Viwanda, shule, maduka na hospital utakaosaidia katika utekelezaji wa maendeleo ya nchi.
Amesema mara ya mwisho kukusanya tafiti za kiuchumi ni mwaka 2015 hivyo, baada ya mafunzo hayo ya siku tano, washiriki watafanya kazi hiyo kwa siku 60 katika mikoa yote.
"Taarifa zitasaidia kuthamini na kuchambua mwenendo wa uchumi, tutajua wamiliki na biashara zao, takwimu zitakuja kutumika katika maendeleo ya nchi,"amesema.
EmoticonEmoticon