JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MIFUGO NA UVUVI
Mji wa Serikali
Mtumba, S.
L. P. 2870, DODOMA.
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Dar es Salaam, Oktoba 16, 2023
UVUMI WA TAARIFA ZINAZOZUNGUKA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII (SOCIAL
MEDIA) KUHUSU UWEPO WA KIWANDA CHA KUTENGENEZA MAYAI, KATA YA GOBA, WILAYA YA
UBUNGO MKOA WA DAR ES SALAAM
Ndugu wanahabari,
Serikali kupitia
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakanusha taarifa za uwepo wa kiwanda cha kutengeneza
mayai katika Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zinazosambazwa
kupitia mitandao ya kijamii. Wizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa imefuatilia
suala hilo kwa kina na kujiridhisha kuwa tarifa hizo sio za kweli, ni
upotoshaji na hivyo kuitaka jamii
kuipuuza.
Ndugu wanahabari,
Kuanzia tarehe 12 Oktoba 2023 kumekuwa na picha ya
mayai mengi na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo
wa kiwanda cha kutengeneza mayai katika Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo Mkoa wa
Dar es Salaam. Picha hiyo
imeambatana na maneno “Serikali Hailali
Kama alivyo Shetani Halali!! Wanajua kabisa Kwa sababu Shetani Halali kwa hiyo
Kuna Mambo Mabaya atayatenda tu!! Kiwanda Cha mayai Goba Kwa wachina
kimekamatwa Sasa hayo Mayai Yote Sijui yametagwa na Kuku Gani? Tusubiri
yanayojiri, Usikie Technologia ilivyo hapo Ndiyo utakapojua Kwa nini kila Mtu
Ana Kitambi”.
Taarifa hizo
zimetengenezwa kwa nia ovu ya kuharibu tasnia ya kuku nchini inayokuwa kwa
kasi. Katika kufuatilia zaidi, Wizara imebaini kuwa picha hiyo ya mayai mengi
iliyotumiwa ilionekana kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2016 na haikupigwa hapa
nchini.
Ndugu wanahabari,
Vilevile, kuna kipande
cha video (video clip) ya kijana anauza mayai ya kuchemsha ambayo yana viini
viwili ambapo baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii wanasema mayai haya
yanatengenezwa viwandani na yanaweza kuwa hatarishi kwa afya ya binadamu. Mayai
yenye viini viwili hayatengenezwi viwandani bali yanatagwa na kuku kama
kawaida. Sababu zinazopelekea yai kuwa na viini viwili ni pamoja na:
(i)
Umri wa kuku, mara nyingi hutokea kwa kuku wanaoanza kutaga
au wanaomalizia umri wa kutaga;
(ii)
Chakula: Wakipewa chakula chenye virutubisho vingi kuku
huweza kuwa na mayai yenye viini viwili;
(iii) Kuwasisimua kuku kwa mwanga
(overphotostimulation);
(iv)
Aina ya kuku
(genetic effects).
Ndugu wanahabari
Viini viwili kwenye
kuku ni sawa na ilivyo mapacha kwa wanyama wengine. Kinachotekea hapa ni kuwa kampuni
za vitotoleshi vya vifaranga hazipendelei kutumia mayai yenye viini viwili kwa
kuwa mayai haya huwa mara nyingi hayaanguliwi, au hata yakianguliwa vifaranga
vitakavyopatikana vinakuwa na uzito mdogo sana au vinakuwa na ulemavu. Hivyo, kampuni
hizo huyabagua mayai yote yenye viini viwili na kuyauza kama mayai ya chakula kama
ilivyoonekana kwenye kipande cha video. Nipende kuwatoa wasiwasi walaji wa
mayai haya kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Ndugu wanahabari,
Naomba kumalizia kuwa
uzushi uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa uwepo wa taarifa ya kiwanda cha
kutengeneza mayai ni upotoshaji na unapaswa kupuuzwa. Serikali inafuatilia kwa
kina aliyeanzisha uhalifu wa taarifa hii na akipatikana Sheria
itachukua mkondo wake.
Asanteni kwa kunisikiliza
Imetolewa
na
Prof. Hezron Emmanuel Nonga
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Simu: 0767238174
Barua pepe: hezron.nonga@mifugo.go.tz
EmoticonEmoticon