Na Karama Kenyunko Michuzi tv
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kuongeza viwango vya utoaji huduma sambamba na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa matumizi mabaya ya viwanja vya ndege nchini.
Amesema viwanja vya ndege havipaswi kuwa vichochoro vya kusafirishia bidhaa haramu kwani itaharibu sifa za nchi na hivyo, kutokuwa miongoni mwa nchi zenye udhibiti wa anga.
Akizungumza leo Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 20 ya TCAA tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003, Waziri Majaliwa amesema mifumo ya udhibiti inapaswa kuimarishwa kwa lengo la kudhibiti na kusimamia huduma za usafiri wa anga nchini.
"TCAA hakikisheni viwanja vya ndege kote nchini haviwi vichochoro vya kusafirishia bidhaa haramu ili nchi iendelee kuwa na sifa ya kuwa kati ya nchi zenye udhibiti wa anga ," amesema Majaliwa.
Pia amesema mamlaka hiyo inapaswa kujifunza kutoka kwa mataifa yaliyoendelea ili kuongeza viwango vya utoaji huduma.
Pamoja na mambo mengine, ameitaka TCAA kuwa wabunifu kwa kuwa na mikakati ya kuimarisha soko ili nchi isiachwe nyuma kimaendeleo.
"Niagize wadau wa usafiri wa anga nchini, mtekeleze majukumu yenu kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia masuala ya usafiri wa anga kitaifa kwa ajili ya kipaumbele namba moja katika usafiri wa anga ni usalama," amesisitiza.
Vilevile aliitaka TCAA kubuni na kuongeza vyanzo vipya vya mapato ya mafunzo ya ndege ili kuongeza idadi ya marubani wanaopata ufadhili wa masomo.
Majaliwa ameagiza Bodi ya Mikopo kufanya marejeo ya viwango vya mikopo vinavyotolewa kwa wanafunzi wa urubani ili kutoa kipaumbele kwa wahitaji wa fani za masuala ya usafiri wa anga.
"Watanzania endeleeni kuviamini na kutumia vyuo vilivyopo nchini kwani vinatoa mafunzo ya uhakika ya utalaamu wa anga wa uhakika," ameeleza.
Majaliwa ameongeza kuwa serikali imepanga kuimarisha sekta ya anga kwa kuwezesha ununuzi wa rada za kisasa nne za kuongoza ndege za kiraia ambazo zimefungwa katika viwanja vya ngege vya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro na Songwe.
"Hivi karibuni, viwanja vya ndege vya Zanzibar na Julius Nyerere vilikaguliwa na kupata asilimia 86.7 hatua hiyo imeowezesha nchi yetu kushika nafasi ya nne badani Afrika ikitanguliwa na nchi ya Nigeria ,Kenya, Ivory Cost, huu ni ushindani tosha kwamba uwezo wa nchi yetu katika kidhibiti usalama wa anga unaendelea kuimarika,"amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewapongeza TCAA Kwa kusimamia ukaguzi huo na kuiweza nchi kupata alama 86.7 katika viwanja vya Dar es Salaam na Zanzibar.
Amesema serikali imeboresha miundombinu mbalimbali ya viwanja vya ndege hivyo kutokana na maboresho hayo anaamino ukaguzi ujao nchi itafikia asilimia 90.
Naye, Mkurugenzi wa TCAA, Hamza Johari, ameeleza kuwa mamlaka hiyo inaendeshwa kwa kutumia mapato ya ndani na kwamba haitegemei ruzuku ya serikali.
"Kwa miaka mitano tumekusanya bilioni 319.9 na bilioni 24.5 tumechangia katika mambo mbalimbali ya kijamii,"amesema Johari
Alisema TCAA imefungua mikataba mbalimbali ya usafiri Kwa nchi 80 hivi karibuni wameingia mkataba na nchi ya Marekani hivyo kuviwezesha ndage ya Air Tanzania kwenda kwenye nchi hiyo.
"TCAA wataacha kusomesha marubani nje ya nchi na kusomesha kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji nchini (NIT) Kwa mwaka tulikuwa tunapeleka marubani 10 nje ya nchi sasa tunasomesha marubani 30 nchini na fedha kubaki nchini,"amesema.
EmoticonEmoticon