NAIBU WAZIRI NDERIANANGA AIKOSHA SHIVYAWATA.

October 23, 2023

 Na Mwandishi wetu - Dar es salaam


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amekabidhi samani za ofisi kwa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mhe. Ummy amekabidhi jumla ya viti vya ofisi (20), meza za ofisi (20) na kabati la ofisi moja, vitabu vya wageni vitano pamoja na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya matumizi ya Ofisi akishirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC). Hafla hiyo imefanyika hoteli ya Lion Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Ummy ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho amesema amefanya uamuzi huo kutokana na changamoto alizozibaini wakati wa uongozi wake hususani uchakavu wa samani za ofisi hivyo kupata msukumo wa kutafuta wadau kuisaidia SHIVYAWATA.

“Ninawashukuru sana TCC kwa support hii na ninaahidi nitaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na SHIVYAWATA katika kuwakwamua, tumekabidhi samani hizi ili mtekeleze majukumu yeni vizuri na nitashirikiana na nyinyi bega kwa bega,” Mhe. Ummy.

Aidha alitoa wito kwa wadau wengine au hata mtu mmoja mmoja kuungana na SHIVYAWATA ili kushirikiana kuboresha Shirikisho hilo katika kukabili changamoto zao na kuwafikia watu wenye ulemavu kwa urahisi pamoja na kuchangia pato la Taifa kutokana na shughuli wanazozifanya.

Katika hatua nyingine SHIVYAWATA wamepokea mchoro wa ramani toka kwa Wakala wa Ujenzi (TBA) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi na ofisi za Shirikisho hilo zitakazojengwa Jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ushirika na Mawasiliano Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Patricia Mhondo amebainisha kuwa moja ya sera za TCC ni kuangalia, kusaidia na kuwezesha miradi yote ambayo ni endelevu na ambayo ni jumuishi wakiwemo watu wenye ulemavu.

" Kwa miaka mingi tumekua tukifanya shughuli kama hizi ambapo takwimu za mwaka huu pekee tumetoa misaada wa vitimwendo zaidi ya 30, fimbo nyeupe zaidi ya 300, Magongo 600, miguu bandia na vifaa vingine" Ameeleza Mkurugenzi huyo.

Naye Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Bw. Ernest Kimaya, mbali na kuishikuru TCC na Mhe. Ummy ametoa pongezi kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kiwanja Jijini Dodoma ambapo ndipo litajengwa jengo la kitega uchumi na ofisi ya Shirikisho hilo.

"Serikali imetusaidia sana ambapo hivi karibuni Mhe. Rais ametupatia kiwanja Jijini Dodoma ili tukae karibu na ofisi za serikali. Pia tunamshukuru Niabu Waziri Ummy kwa kutukumbuka na kurudi nyumbani kutuunga mkono hivyo vifaa hivi vitasaidia ofisi yetu kuwa ya kisasa na tutafanya kazi katika mazingira mazuri,”Ameshukuru Mwenyekiti huyo.

Wakizungumza kwa wakati tofauti washiriki wa hafla hiyo (wenye ulemavu) akiwemo Bw. Hamadi Komboza ameiomba Serikali kuwekeza katika uzalishaji wa visaidizi vya watu wenye ulemavu kupatikana nchini badala ya kuagiza kutoka nje ambapo huletwa kwa gharama kubwa hali inayosababisha wengine kushindwa kumudu gharama hizo.

Naye Bi. Tungi Mwanjala ameipongeza SHIVYAWATA kwa kuendelea kuviunganisha pamoja Vyama vya watu wenye ulemavu hatua inayoleta umoja, mshikamano na upendo baina yao na kujiona ni sehemu ya jamii.

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza  katika hafla ya  makabidhiano ya   samani za ofisi ya  Shirikisho  la Vyama vya  Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jijini Dar es salaam.
 

 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga  akikabidhi picha ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya Shirikisho  la Vyama vya  Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Jijini Dar es salaam.
 

Mkurugenzi wa Ushirika na Mawasiliano  Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC),Patricia Mhondo akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya samani za Ofisi ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Jijini Dar es salaam.
 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga (wa kwanza kushoto) akikabidhi  samani za ofisi kwa  Shirikisho  la Vyama vya  Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Jijini Dar es salaam.
 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bw. Ernest Kimaya (kushoto) akifafanua jambo katika hafla ya makabidhiano ya samani za Ofisi ya Shirikisho hilo na (kulia) ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga Jijini Dar es salaam.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »