WAZIRI BALOZI CHANA ATEMBELEA OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI

September 14, 2023

 NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana ameitaka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa elimu kwa taasisi za umma juu ya taratibu za kisheria wakati wa kuvunja mikataba na kampuni binafsi.

Ameyasema hayo Septemba 13,2023 wakati alipozungumza na menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, baada ya kuwasili katika ofisi hiyo kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema elimu inahitajika ili kuiepushia Serikali hasara ya kulipa fidia kwa makosa mbalimbali ya kisheria.

"Halmashauri, Wizara na taasisi zetu zifanye kazi vizuri, kusiwe na upoteaji wa fedha eti kwa sababu ya kutofuatwa taratibu fulani," amesema.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende amesema kuwa kuvunjwa kwa mikataba pasi ya ofisi yake kushirikishwa ni moja ya changamoto inayoikabili ofisi hiyo.

Dkt. Luhende amesema utaratibu huo wa kuvunjwa mikataba, aghalabu huchagiza migogoro lukuki ya madai ya fidia kwa taasisi za Serikali na wakati mwingine kusababisha hasara.

Pamoja na hayo Dkt.Luhende amezitaja changamoto nyingine zinazoikabili ofisi yake ni baadhi ya taasisi za umma kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi pasi na kuzingatia sheria ambapo hatua hiyo inasababisha kuzaliwa kwa utitiri wa migogoro ya ajira.

Hata hivyo amesema kuwa Ofisi yake inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi wabobevu wa kuendesha mashauri ya migogoro hasa ya Kimataifa na mashauriano katika eneo la mafuta na gesi.

Pamoja na uwepo wa changamoto hizo, amesema mafanikio lukuki yamepatikana ikiwemo kumaliza baadhi ya mashauri nje ya mahakama.

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana akizungumza na menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, baada ya kuwasili katika ofisi hiyo kwa ajili ya kujitambulisha Septemba 13,2023 Jijini Dar es Salaam



Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Pauline Gekul akizungumza wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana alipowasili katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Septemba 13,2023 Jijini Dar es Salaam.




Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akizungumza wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana alipowasili katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Septemba 13,2023 Jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kuzungumza na menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Septemba 13,2023 Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana akiwa na Naibu Waziri Mhe.Pauline Gekul wakipata picha ya pamoja na menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, baada ya kuwasili katika ofisi hiyo na kuzungumza na menejiment hiyo Septemba 13,2023 Jijini Dar es Salaam.


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »