NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Viwango Tanzania limewataka wazalishaji wa Mabati nchini kuzalisha mabati kwa mujibu wa viwango ili kuepuka usumbufu na gharama zisizo za lazima.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Septemba 13,2023 Jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango Bw.Anold Mato amesema bati zinazofaa kwaajili ya kuezekea nyumba ni geji isiyozidi 30.
Amesema bati nyingine zimetengenezwa kwa ajili ya shughuli nyingine kama kutengenezea uzio wakati wa utekelezaji wa miradi, lakini si kwa kuezekea nyumba.
"Mzalishaji wa mabati yenye geji 32 ambayo kwa kawaida ni kwaajili ya uzio, mzalishaji anatakiwa kuweka taarifa ambayo inaonesha kuwa mabati hayo ni kwaajili ya kutengenezea uzio na si kuezekea nyumba". Amesema
Aidha amesema kuwa bidhaa ya mabati imewekwa viwango maalumu vya ubora vinavyostahili kutumika na wazalishaji ambapo bati hutengenezwa kwa chuma na kupakwa madini ya zinki au aluminium zinki ili yawe na uwezo wa kuhimili kutu.
"Viwango vya mabati ni vya lazima na inapotengenezwa inapaswa kuwa na alama ya mzalishaji, kiwango cha madini ya zinki kilichopakwa na geji. Yote haya yaandikwe kwenye bati husika sokoni ili mnunuzi aone na ajue". Ameeleza.
Pamoja na hayo amesema kuwa watumiaji wa mabati inafaa wapate uelewa wa matumizi ya mabati ambapo itasaidia kuepuka hasara zisizo za lazima.
EmoticonEmoticon