PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI AFDP KUNUNUA MELI NANE ZA UVUVI WA BAHARI KUU.

May 17, 2023
Katikati, Mratibu wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Salimu Mwinjaka akiongea na wakurugenzi wa program hiyo, (kushoto) Bw. Robson Mutandi aliyemaliza muda wake na Bw.Boleslaw Stawicki anayechukua nafasi hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe (kulia) akizungumza na Ujumbe na wataalam hawapo katika picha, kuhusu utekelezaji wa Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi, (AFDP) kisiwani humo, kushoto ni Mkurugenzi mpya wa Program hiyo Bw. Boleslaw Stawicki.



K Katikati mhandisi Pius Ntwale, kutoka kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) akionesha Ujumbe kutoka Program ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) pamoja na wataalamu,rasimu ya kwanza ya ramani ya kiwanda cha kuchakata samaki kitakachojengwa katika eneo la Fungurefu katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.





Kushoto Mkurugenzi wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)Bw. Robison Mutandi anayemaliza muda wake akiongea na Mkurugenzi mpya wa Programu hiyo Bw.Boleslaw Stawicki, wakati Ujumbe na wataalam wa Programu hiyo ulipotembea maeneo yanayotekeleza Programu hiyo Kisiwani 

Picha ya pamoja ikionesha baadhi ya washiriki wa mkutano wa ujumbe kutoka AFDP pamoja na
wataalam, wakati ujumbe huo ukiwa katika ziara ya kikazi kisiwani Zanzibar ya kutembelea maeneo
yanayotekeleza mradi huo.
Bi. Jacquline Motcho Afisa kutoka Programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi nchini (AFDP) akizungumza wakati wa mkutano wa wataalamu na ujumbe kutoka AFDP, ulipokuwa katika ziara ya kikazi kisiwani Zanzibar ya kutembelea maeneo yanayotekeleza mradi huo.


Na, Mwandishi wetu – Zanzibar



Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri  Mkuu Sera Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar chini, ya ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), ipo katika hatua za utekelezaji wa ununuzi ya meli nane zitakazotumika katika uvuvi wa bahari kuu kwa Tanzania Bara na Zanzibar.


Hayo yamesemwa Leo 17 Mei 2023, na mratibu wa Progamu ya AFDP Bw. Salimu Mwinjaka, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu alipozungumza na waandishi wa habari  wakati ujumbe wa programu hiyo ulipokuwa kisiwani Zanzibar, katika ziara ya kutembelea maeneo yanayotekeleza programu hiyo.


Bw. Mwinjaka amesema kuwa Programu hiyo ina mpango mkakati unaotekelezwa kwa pamoja na   Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya kilimo na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, ambapo katika utekelezaji wa mpango huo kwa upande wa kilimo, Programu inalenga kuboresha upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima kwa mazao ya alizeti, mahindi na maharage.


Alibainisha kuwa, kwa Upande wa Uvuvi, malengo makuu yapo katika maeneo mawili makubwa ikiwa ni pamoja na uvuvi katika maeneo ya Bahari kuu. “Takribani tunategemea kupata Meli nane (8) ambapo, meli nne zitatumika kwa upande wa Tanzania Bara na Meli nne zitatumika kwa Upande wa Zanzibar.


 Aidha, alibainisha kuwa ili meli hizi zifike kuna mchakato ambao unafanyika ikiwa ni pamoja na upembuzi yakinifu, ili kuona kuwa, meli hizo zitaleta matokeo tarajiwa. Vilevile pia ni lazima kuangalia tathmini ya athari ya mazingira na kijamii na pindi maswala haya yakishakamilika ndipo mchakato wa ujenzi wa Meli hizo utaanza.”  Alifafanua ndugu Mwinjaka.


Sambamba na hilo, Bw, Mwinjaka aliendelea kufafanua kuwa katika kipengele cha upembuzi yakinifu, ndipo itajulikana meli hizo zinatakiwa kuwa na ukubwa na uwezo kiasi gani wa kuchukua na kuhifadhi samaki, na aliongeza kwa kusema kuwa upembuzi huu ukikamilika mapema inatarajiwa kuwa kufikia mwezi June mwaka 2024 meli hizi zitakuwa tayari kwani tathmini ya athari ya mazingira na maandalizi mengine ya awali ikiwa ni pamoja na michoro ya meli hizo imeshakamilika.


Awali, akizungumza katika mkutano uliohusisha ujumbe kutoka katika programu hiyo pamoja na wataalamu, Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dkt Aboud Suleiman Jumbe alisema, kwa upande wa Zanzibar pia Programu hii imejikita katika maeneo mengine matatu ya kuboresha sekta ya uvuvi, ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa samaki, kuboresha miundombinu ya sekta ya uvuvi pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani wa uvuvi na mazao ya baharini.

Ujumbe huo kutoka AFDP na IFAD pia umetembelea mkoa wa Kaskazini Unguja, katika shehia ya mto wa pwani Kijiji Cha Fungurefu, mahala ambapo programu hiyo itaenda kujenga kiwanda cha kuchakata samaki, maghala ya baridi kwa ajili ya kuhifadhi samaki  na mitambo ya kutengeneza barafu, na eneo la Mangapwani pahala ambapo itajengwa Bandari ya Uvuvi.


= MWISHO =


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »