CHAMA cha mchezo wa Wavu Mkoani Tanga (Tareva) kinatarajiwa
kuendesha mafunzo ya waamuzi na makocha yatakayoshirikisha washiriki
kutoa wilaya zote mkoani Tanga na kufanyika kwenye shule ya Sekondari
Tanga School.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Mei 11 hadi 15
mwaka huu yataendeshwa na Mwamuzi wa Kimataifa wa Mpira wa Wavu Saumu
Agapa ambaye anatambuliwa na shirikisho la mpira wa wavu duniani (FIVB)
ambaye atashirikiana na Salim Zuberi kocha mwenye levo ya pili.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwenyekiti wa chama hicho
mkoani Tanga Augustino Agapa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa
ujuzi walimu wa shule za msingi na sekondari.
Alisema baada ya mafunzo hayo anaamini watafanya uamuzi
sahihi kwenye shule zao kwa wale wa msingi na sekondari ambao wakati
mwengine wanaweza kushindwa kufanya hivyo kutokana na kutokutambua
sheria.
Hata hivyo alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni
kuhakikisha mchezo huo unachezwa kuanzia ngazi za chini ili vijana
waweze kukua nao na baadae waweze kupatikana wachezaji wazuri ambao
watakuwa chachu ya mafanikio.
Mafunzo hayo yatawashirikisha walimu wa shule za msingi na
sekondari wanaofundisha michezo vikiwamo vilabu,wachezaji wa zamani
ambao wapo mkoani Tanga.
“Kama unavyojua tumeamua kuanzia mashuleni kwa sababu huko
ndio kisima cha mchezo kutokana na kuwepo kwa vipaji ambavyo vinaweza
kuwa hazina kubwa mkoani hapa kwa siku zijazo”Alisema
