Mchungaji Augustino Simalenga wa
Kanisa la TAG Kivule leo maeneo ya Kitunda akiombea mwili wa marehemu
Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kabla ya kusafirishwa kwa mazishi
yatakayofanyika kesho wilayani ya Rombo.
Msemaji wa familia ya marehemu
Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Silvester Shayo (kulia) akitoa
shukrani kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Wafanyakazi
wa TAA na watu wote walioshiriki kwenye msiba huo. Marehemu Swai
atazikwa kesho wilaya ya Rombo.
Afisa Utumishi Mkuu wa Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Priscus Mkawe
akisoma wasifu wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa
JNIA, kabla ya kuagwa nyumbani kwake Kitunda na kusafirishwa kwenda
Rombo kwa mazishi yatakayofanyika kesho.
Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka
akiaga mwili wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa JNIA, Bw. Jerome Swai,
ambaye atazikwa kesho wilayani Rombo.
Bi. Honoratha Emmilian ambaye ni
mke wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akilia kwa uchungu wakati
wa kuuaga mwili wa mumewe nyumbani kwake Kitunda. Marehemu atazikwa
kesho wilayani Rombo.
Ndugu wa marehemu Jerome Swai
wakiuaga mwili wa mpendwa wao leo nyumbani kwake Kitunda, ambapo
anatarajiwa kuzikwa kesho wilayani Rombo. Swai alikuwa Fundi Sanifu Mkuu
wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Prosper Tesha (mwenye miwani
mbele) akijumuika na waombolezaji kwenye msiba wa aliyekuwa Fundi Sanifu
Mkuu wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw.
Jerome Swai aliyefariki Jumatatu ya wiki hii na atazikwa kesho wilayani
Rombo.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa
Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA), Bw. Jerome Swai likipandishwa ndani ya basi tayari kwa safari ya
kwenda Rombo kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho. Marehemu
aliajiriwa mwaka 1984.
……………..
Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa Kanisa la TAG Kivule,
Augustino Simalenga amewataka wanadamu kujiandaa na kumrudia muumba wao
kwani hawajui siku wala saa watakapokufa.
Alitoa kauli hiyo leo kwenye
misa ya kumuaga marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), iliyofanyika
nyumbani kwake maeneo ya Kitunda, ambapo amewataka watu kujiandaa mapema
kwa kuwa hawajui watakapokwenda baada ya kifo.
“Neno la Mungu linatukumbusha
kuwa tujiandae mapema, ndugu yetu Jerome ameshamaliza kazi, tunatakiwa
kujitafakari sisi hatima yetu itakuwaje, kwani wapo waliolala mauti
Biblia inasema hao wanapumzika wakisubiri siku atakaporudi Mwana wa Adam
atakuja kuwachukua wote waliohai na wale waliokufa wakimuamini Kristu
watafufuliwa kwanza ili kwa pamoja wamlaki Bwana wao mawinguni,” alisema
Mchungaji Semalenga.
Alisema kila mtu atafakari
maisha ya hapa duniani kwani mlango wa kutokea hapa duniani aidha ni
kifo au siku Bwana atakapokuja kuchukua watu wake, hivyo ni vyema
kujiandaa kwa kutafakari maisha baada ya hapa kwa sasa kuanza
kujitengenezea hazina mbinguni.
“Ukisoma kitabu cha Mhubiri
sura ya 3 utaona Mungu ameweka kila kitu na wakati wake, upo wakati wa
kula na wakati wa kusema, wakati wa kunyamaza, wakati wa kuzaliwa na
wakati wa kufa kila kitu kinawakati hata sisi tuliohai ni wakati wetu
kuwa hai bali utafika wakati hatutaweza kuwa hai siku zote, na kila
jambo lina mwanzo na mwisho, lakini mwisho wa jambo unatengenezwa wakati
wa sasa kama maisha yetu ya sasa hatufikiri mwisho basi tukifika mwisho
tutakuwa watu wa kujuta, watu wa kuomboleza na lakini sasa Mungu
anatupa nafasi ya kuyakabili mambo yanayokuja na hatima ya maisha yetu,”
alisisitiza.
Alisema katika kitabu cha
Zabuni, kinasema binadamu amepewa maisha mafupi na machache, na kuishi
ni miaka 70 na wachache wanaweza kuishi zaidi ya hiyo, ambapo ni tofauti
na wanadamu wa kwanza waliishi miaka 100 ambayo nayo yalikuwa mafupi.
Hata hivyo alisema baada ya kifo yapo maisha ya milele, ambayo mwanadamu
anatakiwa kuyatafakari sasa kwa kujiwekea hazina itakayomwezesha kuishi
vyema mbinguni.
Mchungaji Simalenga alisema
amefanya utafiti katika huduma anazotoa lakini amegundua hakuna
mwanadamu anayetaka kwenda jehanamu, hata asiyefanya ibada kwa Mungu
anamatumaini ya kwenda mahala pema peponi.
“Mungu ameweka utaratibu na
Mwanadamu akiuufuata ndio atafikia kwenye ule mpango ambao Mungu
ameuweka, sasa kama hataki kuufuata anajikuta siku za maisha yake
atajikuta mahala asipotaka kwa kilio, kujuta na kuomboleza, kwani
alikuwa akipuuzia na kuona mambo ya Kimungu ni ya kiduni na watu maskini
na wachini, wakati ni mambo ya msingi kuliko kitu chochote duniani,”
alisema Mchungaji Simalenga.
Naye Afisa Utumishi Mkuu wa JNIA,
Bw. Priscus Mkawe alisema marehemu Swai ameacha pengo kubwa kutokana na
umahiri wake katika utendaji kazi wake uliotukuka.
“Marehemu Swai alikuwa mmoja wa
wafanyakazi wa kipekee aliyefanya kazi kwa bidii na kujituma na kutokana
na uchapakazi wake aliwahi kuchaguliwa kuwa mfanyakazi hodari kuanzia
mwaka 2001, 2003 na 2017, hivyo JNIA na TAA kwa ujumla tumempoteza
mfanyakazi hodari sana,” alisema Priscus.