Na: Veronica Kazimoto-Sirari
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere amewataka
Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali wakiwemo wa mamlaka hiyo wanaofanya
kazi katika Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari kilichopo wilaya ya
Tarime mkoani Mara kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha
wanaendelea kutoza kodi stahiki.
Akizungumza
wakati wa ziara yake kituoni hapo, Kamishna Mkuu Kichere alisema nchi
inaendeshwa kwa kodi za ndani hivyo ni muhimu kila taasisi iliyopo eneo
hilo kutimiza wajibu wake katika suala zima la ukusanyaji wa kodi.
“Wote
mnajua umuhimu wa kodi na pia mnafahamu kuwa, kwa kupitia kodi hizi,
Serikali inajenga miundombinu ya barabara, umeme, inasomesha wanafunzi,
inajenga shule, inalipa mishahara ya wafanyakazi wake na mambo megine
mengi. Hivyo, mfanye kazi kwa bidii na kwa weledi ili mkusanye kodi
inayotakiwa kukusanywa kwa mujibu wa sheria bila kumuonea mtu yeyote.”
alisema Kichere.
Kichere
aliongeza kuwa, wafanyakazi wote kituoni hapo wana wajibu wa kukusanya
kodi ili kuisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo kwa kutumia mapato
yanayokusanywa nchini kupitia kodi mbalimbali.Aidha,
Kamishna Mkuu huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara na Kamati yake ya
Ulinzi na Usalama pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano
wanaoutoa kwa TRA.
“Nachukua
fursa hii kukushukuru wewe Mhe. Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati yako ya
Ulinzi na Usalama na pia napenda kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Tarime
Mhe. Glorious Luoga kwa ushirikiano mkubwa mnaoutoa kwa Mamlaka ya
Mapato Tanzania,” amesema Kichere.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima alisema kwamba, mkoa
wake umepanga utaratibu wa kufanya kikao kila mwezi ili kupitia taarifa
ya ukusanyaji mapato mkoani humo.
“Kwa
mkoa wa Mara kituo hiki cha Sirari ni muhimu sana na kina maslahi
makubwa hususani katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, hivyo sisi
kama mkoa tumejipanga kila mwezi kukaa pamoja kupitia taarifa ya TRA ili
kupata viashiria vya maeneo muhimu ya ukusanyaji mapato ndani ya mkoa
wetu,” alisema Malima.
Naye
Kaimu Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mkoa wa Mara Laurent Kagwebe
ameushukuru uongozi wa mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa
katika suala zima la ukusanyaji mapato mkoani humo na kusema kuwa
ushirikiano huo ukiendelea, kuna dalili njema za kuongezeka kwa
makusanyo hapo baadae.
“Nikili
wazi kuwa, nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa Mkuu wa
Mkoa na Wakuu wa Wilaya mkoani hapa na kama ushirikiano huu ukiendelea,
nina imani kuwa, makusanyo yataongezeka kwa kiasi kikubwa,” amefafanua
Kagwebe.
Kituo
cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari kina jumla ya wafanyakazi 86 kutoka
taasisi mbalimbali za Serikali ambapo pamoja na mambo mengine,
wafanyakazi hao wana jukumu la kulinda afya za wananchi kwa kukagua
bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia kituo hicho, kulinda usalama wa raia
pamoja na kukusanya mapato ya Serikali.