Waziri Wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari
hawapo pichani kuhusu mambo mbalimbali serikali iliyozungumza na Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani Gianni Infantino na Rais wa CAF
Ahmad Ahamad alipokuwa nchini kwa ajili ya mkutano wao leo jijini Dar es
Salaam.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania Wallace Karia akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari
kuhusu hali ya kifedha kwa shirikisho hilo na matarajio baada ya FIFA
kuwapa maelekezo ya kufuatilia fedha ambazo hawakuingiziwa kutokana na
matatizo ya viongozi waliyopita leo jijini Dar es Salaam.
……………….
Na Anitha Jonas –WHUSM
Dar es Salaam.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
kuendeleza viwanja tisa nchini kufuatia kuongezeka kwa dau la pesa za
Maendeleo na Kujiendesha zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Duniani FIFA kuanzia mwaka 2019 .
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
Dkt.Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu
mambo mbalimbali serikali iliyojadili na Rais wa FIFA Gianni Infantino
alipokuwa nchini kwa mkutano wake hivi karibuni.
‘’Rais wa FIFA alieleza kuongeza
mara nne ya kiwango cha pesa za maendeleo na kujiendesha walizokuwa
wanatoa kwa mashirikisho kama TFF mpaka kufikia Dola Milioni Moja na
Laki Mbili na Nusu kwa mwaka na kusema pesa hizo ndiyo zitumike
kuendeleza viwanja vya michezo kwani uwepo wa viwanja ndio unaosaidia
kukuza vipaji vya soka,’’alisema Dkt.Mwakyembe.
Akiendelea kuzungumza katika
mkutano huo na waandishi wa habari Waziri Mwakyembe alisisitiza kuwa
Rais huyo wa FIFA ametoa msisitizo wa kutokuwa na huruma kwa kiongozi
yoyote wa shirikisho atakayekuwa na matumizi mabaya ya pesa pamoja na
kufanya udanganyifu kwani yeye yuko mstari wa mbele kupinga ufisadi
katika sekta ya maendeleo ya Soka duniani.
Pamoja na hayo nae Rais wa TFF
Bw. Wallace Karia alitoa ufafanuzi wa hali ya kifedha kwa shirikisho na
kueleza kufuatia kuwepo na matatizo katika shirikisho hilo FIFA ilikuwa
imesitisha kuwapatia fedha hizo za maendeleo na kujiendesha tangu mwaka
2015 lakini baada ya kuingia uongozi mpya ambao FIFA wameridhika nao na
wameshaupa utaratibu wa kufuatilia fedha hizo.
‘’Rais wa FIFA alitueleza kuwa
fedha hizo ziko salama nchini Zurich ni kwamba tu hazikuwa zimeruhusiwa
kuingia nchini na kwa sasa tumeshaanza mchakato wa kufuatilia fedha hizo
kwa kuzingatia maelekezo ya FIFA hivyo basi tutakapo pata fedha hizo
Shirikisho litaendeleza baadhi ya miradi ambayo tumekwisha
iandaa,’’alisema Bw. Karia.
Pamoja na hayo rais huyo alitoa
wito wa wakazi wa jiji la Tanga waliyovamia eneo linalotarajia kujengwa
Technical Center ya mchezo wa soka basi waondoke mara moja kabla
hawajachukuliwa hatua.(Chanzo Fullshangweblog)