Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya
Lushoto (DCC) imeamua kusitisha mpango wa ujenzi wa jengo la Halmashauri
ya Bumbuli lilokuwa lijengwe kwenye eneo jipya la Kwehangala hadi hapo suluhu
ya mgogoro baina ya viongozi wa halmashauri hiyo itakapopatikana.
Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto January Lugangika (Pichani Juu) alisema kuwa maamuzi hayo
yamefikiwa baada ya kuwepo sintofahamu kati ya Madiwani wa halmashauri hiyo na
viongozi wengine juu ya suala hilo. .
Hivi karibuni kumekuwepo na mvutano
mkubwa kati ya viongozi hao juu ya wapi pajengwe majango ya makao makuu ya
Halmashauri hiyo.
Baadhi ya viongozi wanadai
utaratibu wa fedha za manunuzi haukufuatwa katika kufikia maamuzi ya
kujenga jengo la Halmashauri katika eneo la Kwehangala na kuacha majengo
yaliyokwisha jengwa Bumbuli kwa gharama ya Sh. milioni 700.
Kutokana na mvutano huo, Mkuu
huyo wa Wilaya amesema kikao kiliafiki kisitishe zoezi hilo mpaka
maelewano yatakapopatikana.
" Wajumbe wameshauri suala
la kuhamisha makao makuu lisitishwe hadi hapo utakapopatikana
utangamano,kwani tayari imeonekana kuna mgogoro ambao umeleta utengano kwa
viongozi" Alisema Lugangika .
Mbunge wa jimbo hilo, January
Makamba alikiri kuwepo kwa mvutano huo ambao alisema hauna tija katika
kuwaletea maendeleo wananchi wa Bumbuli.
Makamba alisema ni vyema kama
viongozi wakazungumzia suala la maendeleo mfano;maji,barabara,umeme,nyumba za
watumishi badala ya kila siku kuzungumzia wapi kujengwe jengo la halmashauri.
Alishauri kuwa wananchi
washirikishwe katika suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kutosha juu
ya hoja ya kuhamisha halmashauri kwa kuwa ndio wenye chombo chao badala ya
viongozi kuamua wao pekee.
"Suala hilo nakubaliana na
maoni wa kikao cha DCC tulisitishe kwani kwa sasa hatuna shida na majengo ya
halmashauri kwa sababu majengo tunayo ambayo hatulipii kodi ya pango. Sasa hivi
tuzungumzie maendeleo kwani wananchi mwaka 2020 hawatatudai majengo ya
halmashauri bali watatudai maendeleo juu ya huduma muhimu za jamii alisema
Makamba.
Hivi karibuni baadhi ya Madiwani wa
Halmashauri hiyo walipiga kura ya kupitisha azimio la kujenga jengo hilo
la halmashauri huku Madiwani nane wakigoma kupiga kura kwa madai kuwa hawawezi
kupiga kura wakati kuna ukiukwaji wa kanuni na utaratibu ktk kitengo cha
manunuzi.
Madiwani hao nane ambao waligoma
kupiga kura kupitisha azimio hilo mnamo January 18 mwaka huu walimuomba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kuingilia kati mgogoro na kuzuia
walichokiita ukiukwaji wa utaratibu wa manunuzi pamoja na maelekezo
mbalimbali ya viongozi juu ya mpango huo.
Pia walimuomba aingilie kati na
kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma na ukiukwaji wa
utaratibu wa uendeshaji wa halmashauri na kudharau kwa makusudi maelekezo
yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa serikali kuu.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amir
Shehiza alisema kuwa baraza ni chombo chenye maamuzi sahihi
hivyo alikitaka Kikao hicho cha DCC kuacha kuingilia Kazi za baraza
.