Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Joelson Mpina akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anarozy Nyamubi baada ya kuteketeza nyavu haramu katika Wilaya ya Butiama leo. (Na John Mapepele) |
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vincent Anney akimwaga mafuta kwenye nyavu haramu ili kuzichoma moto katika kijiji cha Bwai Kumusoma wilayani Musoma leo. (Na John Mapepele) |
Asisitiza operesheni ya kutokomeza
uvuvi haramu kanda ziwa ni ya kudumu
Na John Mapepele, Mara
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameagiza viwanda
vinne vya kuchakata samaki na mazao yake vilivyofungwa katika
Mikoa ya Mwanza na Mara kuanza kazi mara moja ifikapo Julai Mosi mwaka
huu, ambapo amewataka wamiliki kupeleka mipango kazi ya namna ya
kuvifufua kabla ya kufikia mwezi Machi mwaka wizarani kwake.
Alivitaja viwanda
hivyo kuwa ni Tan Perch Limited na Supreme Perch Limited vilivyopo Mwanza
na Mara Fish Packers Limited na Prime
Catch Limited katika mkoa wa Mara.
Waziri Mpina alizungumza hayo jana wakati alipokuwa kwenye
ziara ya kikazi mkoani Mara na Mwanza kukagua operesheni maalum ya kutokomeza
uvuvi haramu kanda ya Ziwa Victoria inayofanywa na kikosi kazi maalum
alichokiunda hivi karibuni.
“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Sekta ya Uvuvi nchini
niliyepa kulinda raslimali za uvuvi nitahakikisha kwamba ulinzi wa raslimali hizi ni wa kudumu, na
usio na mwisho hadi uvuvi haramu utakapoisha
hapa nchini” alisisitiza Mpina
Waziri Mpina alipata fursa ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Mara na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo, wananchi katika maeneo tofauti na
hatimaye kushiriki katika zoezi la kuchoma nyavu haramu ambapo hadi sasa zaidi
ya nyavu zenye thamani ya shilingi bilioni nne zimechomwa moto katika zoezi
linaloendelea la kudhibiti uvuvi haramu mkoani Mara.
Kamanda anayeongoza kikosi cha kupambana na kudhibiti uvuvi
haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi Kanda ya Mara, Bakari Lulela alimweleza
Waziri Mpina kuwa operesheni hiyo imefanyika katika Wilaya za Musoma, Butiama,
Rorya na Bunda na kufanikiwa kukamata na kuteketeza zana haramu zenye thamani
ya sh. bilioni 3.2 huku wavuvi na wafanyabiashara wa samaki na mazao yake
waliokiuka sheria ya uvuvi wakitozwa faini ya sh. milioni 189.
Waziri Mpina aliziagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia
hatua Maafisa Uvuvi wa Kijiji cha Bwai Kumsoma waliotuhumiwa kushirikiana
na wavuvi haramu kuondolewa mara moja katika kijiji hicho ili kupisha uchunguzi
na ikithibitika wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vincent Anney amesema kwamba
hayuko tayari kuona Wilaya yake inaendelea kuishi na watumishi wanaojihusisha
na uvuvi haramu na kwamba sheria kali
zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika wilaya hiyo.
Aidha Waziri Mpina ameiagiza Wizara yake kuandaa bei elekezi
ya kununua samaki itakayowezesha kuondokana na tabia ya wenye viwanda kushusha
hovyo bei pindi samaki wanapoongezeka na hivyo kuwadhulumu wavuvi kupata malipo
stahili yanayotokana na kazi yao.
Waziri Mpina alisema Ziwa Victoria ni hazina na raslimali
kubwa kwa Tanzania ambapo inaaminika kuwa
ni la kwanza kwa ukubwa katika bara la Afrika kwa kuwa na eneo la
68,000Km2 na la pili duniani.
Alisema pamoja na umuhimu wa ziwa hili katika kukuza uchumi
na kuboresha maisha ya watanzania bado linakabiliwa na shughuli za uvuvi haramu
uliokithiri ambapo tafiti zinaonyesha kwamba kama hakutakuwa na jitihada za
haraka za kutokomeza uvuvi haramu, ziwa hilo hali halitakuwa na raslimali za uvuvi ikiwa ni pamoja na
samaki katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Alitaja uvuvi haramu unaofanywa kuwa ni pamoja na kuvua katika maeneo
yasiyoruhusiwa, kutumia valiyombo visivyosajiliwa, kuvua bila leseni,kutumia
sumu, kutumia nyavu za utali na kuvua samaki wachanga ama wazazi wasioruhusiwa.
Uvuvi haramu mwingini nikuvua kwa kokoro na nyavu zenye macho madogo chini ya kiwango
kinachokubalika kisheria, katuli, kumbakumba na gizagiza ambapo alisema
Serikali imedhamilia kutokomeza uvuvi
huo haramu.
Aidha alisema operesheni hiyo katika kanda ya Ziwa Victoria
dhidi ya uvuvi haramu ni ya kudumu na inafanyika kwa
kuzingatia Sheria ya Uvuvi Na.22 yaMwaka 2003 na Kanuni 58(1) ya Uvuvi ya Mwaka
2009 na Sheria ya Mazingira Na 20 ya Mwaka 2004 kifungu Na(1), 65(1)a pia
Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Na 29 ya Mwaka 1994 ili kudhibiti
uvuvi haramu ulioshamiri kiasi cha kutoweka kwa raslimali ya samaki katika ziwa
hilo kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Waziri Mpina alisema Tanzania inamiliki 51% ya Ziwa hili
ikifuatiwa na Uganda 43% na nchi ya Kenya inamiliki 6%. Ziwa hili ni moja ya
maziwa yanayozalisha samaki kwa wingi duniani kwa makadirio ya takribani tani
1,000,000 kwa mwaka ambapo asilimia 60
ya uzalishaji wa samaki wake unatoka Tanzania hivyo juhudi za pamoja za
kutokomeza uvuvi haramu zinahitajika.