Mkurugenzi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT),(kulia), anaeshughulikia masuala ya kibenki Bw. Kened
Nyoni na Kaimu Kamishna Msaidizi Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. Michael Nyagoga (Kushoto) wakifuatalia mada mbalimbali zilizokuwa
zikitolewa katika mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi
(COBAT), uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini
Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Benki za Wananchi Tanzania (COBAT), Bw. Mugwagi Stephen akizungumza
katika mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi uliofanyika
kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma. Kulia kwake ni
Mweyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mhe. Hawa Ghasia na Kushoto
kwake ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).
Mbunge wa Mtwara Vijijini ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa Ghasia
akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) ili aweze kufungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya
Benki za Wananchi kwaniaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa,
uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akihutubia katika mkutano maalum wa wadau
wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, uliofanyika mjini Dodoma ili
kujadili masuala ya Mitaji na Mpango wa Kuziunganisha Benki za Wananchi
Tanzania.
Washiriki wa mkutano maalum wa
wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi wakifuatilia matukio mbalimbali
wakati wa mkutano huo uliofunguliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), kwa niaba ya Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Mjini Dodoma.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Dkt. Benard Kibesse (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa
Jumuiya ya Benki za Wananchi –COBAT, Bw. Rukwaro Senkoro, wakisikiliza
kwa makini hotuba ya Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, iliyosomwa kwa
niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
(Mb), mijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akifurahia jambo na Mbunge wa
Mtwara Vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Bajeti Mhe. Hawa Ghasia baada ya kufungua mkutano wa wadau wa Jumuiya
ya Benki za Wananchi-COBAT, uliofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha
na Mipango mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa Nne kushoto), akiwa katika picha ya
pamoja na wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, uliofanyika
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akibadilishana mawazo na baadhi
ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioshiriki
mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, nje ya Makao
Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana
na Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi-COBAT, Bw.
Rukwaro Senkoro, nje ya Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango mjini
Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
……………………………………………………………………………..
Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania BOT kuzifutia
leseni benki zote za biashara pamoja na benki za wananchi
zitakazoshindwa kukidhi vigezo vya kuendesha shughuli za kibenki nchini.
Ametoa
agizo hilo mjini Dodoma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua Mkutano
Maalum wa Wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT).
“kwa
taarifa niliyonayo hadi sasa baadhi ya benki hazijatimiza matakwa ya
kisheria ya kuwa na mtaji wa kutosha, hali ambayo haiwezi kuachwa
iendelea hata kidogo, kwani haiimarishi sekta ya fedha na haiwasaidii
wananchi kuendelea kiuchumi” alisema Waziri Kassim Majaliwa katika
hotuba hiyo
Alisema
Benki Kuu ilitoa muda hadi mwishoni mwa Desemba 2017, benki za wananchi
ziweze kuongeza mtaji na kwamba muda huo hautaongezwa na wala Serikali
haitatoa mtaji kwa benki hizo.
“Serikali
kupitia Benki Kuu ya Tanzania haitasita kuifungia benki yoyote na
kufuta leseni yake ya biashara pindi itakapobaini inavunja sheria, ikiwa
ni pamoja na kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi ambao
unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na amana za wateja kama
tulivyofanya kwa Mbinga Community Bank PLC kuanzia tarehe 12/5/2017”
alisema Dkt. Mpango kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Maagizo
hayo yamekuja siku moja baada ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango wakati akifungua tawi kuu
la Benki ya CRDB mjini Dodoma, kuhakikisha kuwa Benki Kuu ya
Tanzania-BOT, inazifuta benki zote zinazoshindwa kujiendesha kibiashara
hata kama zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Alisema
Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha benki za wananchi
zinaimarika zikiwemo kuruhusiwa kuanzisha mifumo ya ushirikiano katika
Nyanja ya Mfumo wa Mawasiliano na Habari (ICT), Idara za Ukaguzi wa
Ndani (Internal Audit Services), kupunguza wingi wa idara na kuwa na
idara tatu (3) tu muhimu, kuruhusiwa kuungana (Federation), ambazo
zitapunguza gharama za uendeshaji wa benki za wananchi na kuleta ufanisi
katika kutoa huduma.
“Napenda
kusisitiza kuwa sekta ya benki ni muhimu sana kwa uhai na ukuaji wa
uchumi kama ilivyo damu kwa mwili wa binadamu na kutokana na umuhimu
wake huo, sekta hii ni kati ya sekta chache zinazosimamiwa kwa karibu
sana ili kulinda amana za wateja pamoja na kuhakikisha uhimilivu wa
mfumo mzima wa sekta ya fedha na mwenendo wa uchumi wa Taifa” aliongeza
Dkt. Mpango
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT) Bw. Rukwaro Senkoro, alisema hadi
kufikia Juni, 2017, Benki za Wananchi nchini zilikuwa na wateja zaidi
ya milioni 1.4, wateja wa vikundi zaidi ya 10,000, Matawi 12, Vituo 59,
na wanahisa 66,492.
“Benki
hizo zina amana zenye thamani ya shs bilioni 74.2, zimetoa mikopo ya
sh. bilioni 56.8, na jumla ya mali zenye thamani ya shs. bilioni 92.3”
Alisema Bw. Senkoro
Hata
hivyo, kutokana na Utafiti wa Matumizi ya Huduma za Kifedha uliofanyika
mwaka 2017 umebaini kuwa asilimia 28 ya wananchi bado hawapati huduma
za kifedha hapa nchini hususan vijijini na kutaja changamoto ya ukosefu
wa mitaji ya benki hizo kukwaza sekta hiyo.
Dhana
kuu ya mkutano huo wa COBAT uliowashirikisha wadau mbalimbali kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar ni “Mitaji na Mpango wa Kuziunganisha Benki za
Wananchi Tanzania”, ambayo ni dhana mpya.