WAHAMIAJI HARAMU 224 WAKAMATWA MKOANI TANGA

December 25, 2017
ZAIDI ya  wahamiaji haramu 200 wamekamatwa mkoani Tanga kufuatia operesheni zilizokuwa zikifanyika na Jeshi la Polisi kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu kutokana na kuingia nchini kinyume cha sheria.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna  Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi  hilo, Edward Bukombe (Pichani kushoto) wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema wahamiaji hao walimatawa maeneo mbalimbali mkoani hapa.

Aliwataja wahamiaji ambao walimatwa kuwa ni 55 raia kutoka nchini Somalia,Waethiopia walikuwa 149 na Wakenya walikuwa 20 ambapo alitoa wito kwa watanzania wanaoshirikiana nao kuwaingiza hapa nchini kuacha mara moja vitendo hivyo kabla hawajakumbana na mkono wa kisheria.

“Wahamiaji hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali kufuatia operesheni ambazo zilikuwa zikifanyika lakini niwatake watu wanaoshiriki kuwaingiza wahamiaji haramu hao kuacha biashara hivyo mara moja na watafute nyengine kwani hawatakuwa salama watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria “Alisema RPC.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha 14 kwa kipindi cha mwaka  mzima wakati wa operesheni ikiwa ni mkakati wa kudhibiti matukio ya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha mkoani hapa.

“Katika operesheni hizo tulikamata  Pistol 2,Shortgun 3,Gobore 9
ambazo bila shaka hizi kwa namna moja ama nyengine zingeweza kutumika katika masuala mbalimbali ya uhalifu “Alisema.

Hata hivyo alisema Jeshi la Polisi limejipanga imara kuweza
kuhakikisha linazibiti vitendo viovu vinavyoweza kusababisha kutoweka kwa amani kwenye maeneo yao kwa kuwachukulia hatua watu ambao watabainika kuhusikaa navyo.

“Sisi kama Jeshi la Polisi hatujalala tupo macho kila wakati
kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani kwenye maeneo yao na wale ambao watakuwa chanzo cha kusababisha amani kutoweka tutakula nao sahani moja kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya dola “Alisema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »