JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA FEDHA NA MIPANGO
TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU MATUMIZI YA FEDHA ZA KIGENI KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza
kuwa utekelezaji wake uanze tarehe 1
Januari, 2018. Maagizo hayo ni kama ifuatavyo:
-
i.
Bei zote hapa nchini
zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za
kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya
usafiri na vifaa vya kielektroniki.
ii.
Bei ambazo walengwa
wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za
kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi
zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania,
gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na
viza kwa wageni, na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji
wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za
kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.
iii.
Viwango vya
kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili
viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na
maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha
fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
iv.
Mkazi yeyote wa
Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za
kigeni.
Aidha Dkt. Mpango
ameviagiza vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote
watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA
YA FEDHA NA MIPANGO