Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango (Mb) , akitolea ufafanuzi masuala kadhaa yanayohusu
changamoto za kodi katika Sekta Binafsi wakati wa mkutano kati ya
Serikali na Sekta hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango mjini Dodoma
Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya
Sekta Binafsi nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye
viwanda nchini CTI, Dkt. Samuel Nyantahe akizungumza jambo wakati wa
mkutano kati ya Serikali na Sekta Binafsi uliofanyika mjini Dodoma.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango
…………..
Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amewaahidi wafanyabiashara na
wawekezaji nchini kwamba serikali italifanyiakazi suala la kodi katika
Bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019 ili kuboresha zaidi mazingira ya
uwekezaji na biashara kupitia sekta binafsi.
Dokta
Mpango ameyasema hayo mjini Dodoma katika mkutano wa tatu kati ya
Serikali na Sekta binafsi ambapo masuala mbalimbali yanayohusu kodi
yamejadiliwa ikiwa ni mwendelezo wa Serikali kutaka kuiimarisha Sekta
hiyo ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Alisema
kuwa Serikali imedhamiria kupunguza ama kuondoa kabisa kero
zinazoikabili sekta binafsi ikiwemo malalamiko ya muda mrefu ya utitiri
wa kodi ili sekta hiyo iweze kuwa na nguvu na kushiriki kikamilifu
katika kujenga uchumi wa viwanda utakaokuza pato la taifa na ajira
nchini.
Alisema
Serikali inatambua kwamba sekta binafsi ndiyo nguzo ya ukuaji wa uchumi
wa Taifa ndio maana inajitahidi kupata maoni ya wadau kuhusu namna ya
kuboresha mazingira yao ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili
kuharakisha maendeleo ya nchi.
“Ni
lazima dukuduku za sekta binafsi tuzisikilize, tuzitafakari na
kuzifanyia kazi ili uchumi uweze kwenda kwa kasi zaidi tuwaondoe
wananchi wetu kwenye umasikini na vijana wetu wapate kazi’ Alisema Dkt.
Mpango.
Alisema
wakati wa kuandaa bajeti yam waka 2018/2019, serikali itaweka mfumo wa
kodi utaoiwezesha Sekta Binafsi kukua na kuimarika zaidi ili iweze
kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya watanzania kwa
ujumla.
“Katika
mjadala huu nimefurahia kusikia maoni ya sekta binafsi ambapo pamoja
na kupendekeza maeneo ya kupunguza kodi, lakini pia wamezungumzia namna
ya kuongeza wigo wa kuongeza mapato ya Serikali” Aliongeza Dkt. Mpango.
Hata
hivyo, Dkt. Mpango, alitahadharisha jumuiya ya wawekezaji na
wafanyabiashara nchini kwamba wanapojadili juu ya masuala ya kodi,
wakumbuke kwamba Serikali ina mzigo mkubwa wa kuhudumia jamii katika
masuala mbalimbali ikiwemo elimu, maji, afya, barabara, miundombinu ya
usafiri na usafirishaji ikiwemo reli na mingine mingi.
Alitolea
mfano uzalishaji wa maji katika miji mikuu ya Wilaya na miji midogo ni
lita milioni 99.5 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 273 kwa siku,
sawa na 36.4%.
“Miradi
ya maji ya Kitaifa uzalishaji ni lita milioni 59.5 ikilinganishwa na
mahitaji ya lita 119 kwa siku, sawa na 50% ya mahitaji” Alisisitiza Dkt.
Mpango
Alibainisha
kuwa vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 katika kila vizazi hai 100,000
wakati lengo ni kuvipunguza visizidi vifo 265 katika kila vizazi hai
100,000 itakapofika mwaka 2020.
Aidha
Dkt. Mpango alisema kuwa huduma za msingi zinazotolewa na Serikali
hususan, ulinzi wa nchi, usalama wa raia, na mali zao, utawala,
usimamizi wa rasimali za nchi, na ujenzi wa miundombinu ya msingi isiyo
na mvuto kwa sekta binafsi, lazima ziendelee kugharamiwa na Serikali.
Dkt.
Mpango alielezea pia namna misaada na mikopo kutoka kwa wadau wa
maendeleo inavyopungua mwaka hadi mwaka ambapo alisema mikopo yenye
masharti nafuu ilishuka kutoka shilingi trilioni 1.3 mwaka 2013/14 hadi
shilingi bilioni 495 mwaka 2015/2016
Alifafanua
kuwa misaada kutoka kwa washirika hao wa maendeleo imeshuka kutoka
shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka 2013/2014 hadi sh. Trilioni 1.23 mwaka
2015/2016.
Vilevile
alieleza kuwa kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari miongoni mwa
wafanyabiashara na wawekezaji bado hakiridhishi na ukwepaji kodi/uvujaji
wa mapato ya Serikali bado ni matatizo sugu hivyo kuitaka Sekta Binafsi
iyatupie macho mambo hayo wakati wakijadili na kushauri namna Serikali
inavyoweza kuboresha kodi ili mambo hayo ya msingi ya kuihudumia jamii
yasikwame
Wakizungumza
kwa niaba ya Sekta Binafsi, Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda
hapa nchini Dokta Samuel Nyantahe na mmoja wa wafanyabiashara Bw. Boaz
Ogola, wameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa nia yake ya dhati ya
kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara hapa nchini na
kwamba wako tayari kushirikiana nayo ili kutimiza azma yake ya kufikia
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kuwa wameiona nia njema ya
Serikali ya kufikia hatua hiyo
Mkutano
huo wa siku moja umewakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka
ndani na nje ya nchi huku agenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kujadili kwa
undani masuala mbalimbali ya kodi ambapo Sekta binafsi imependekeza
mambo kadhaa ambayo Serikali imeahidi kuyafanyiakazi.