EfG YAZINDUA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA JIJINI DAR ES SALAAM

December 01, 2017
 Mkurugenzi wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Jane Magigita akihutubia katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliofanyika Dar es Salaam jana Soko la Tabata Muslim.
 Mratibu wa Mradi wa Mpe Riziki Si Matusi, Susan Sita akimpatia fulana Mwakilishi wa Mbunge wa Segerea, Bonah Kaluwa aliyefika kwaniaba yake kama mgeni rasmi, Shanisudin Ahmed wakati wa uzinduzi huo.
  Mkurugenzi wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Jane Magigita, akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi.
 Mwenyekiti wa Soko la Tabata Muslim, Haji Mohamed akihutubia.
 Mratibu wa Mradi wa Mpe Riziki Si Matusi, Susan Sita, akihutubia.
 Wawezeshaji wa kisheria wa EfG wakiwa na furaha katika uzinduzi huo.
 Burudani ikitolewa.
 Burudani ikiendelea.


 Mkurugenzi wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Jane Magigita akihutubia
 mgeni rasmi, Shanisudin Ahmed, akihutubia wakati wa uzinduzi huo.
 uzinduzi ukiendelea.
 Wadau mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo
 Mkurugenzi wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Jane Magigita akiteta jambo na mgeni rasmi.
Mgeni rasmi akijumuika na wadau mbalimbali na wawezeshaji sheria wa shirika hilo.

Na Dotto Mwaibale

SHIRIKA la Equality for Growth (EfG) lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam, jana limezindua siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kama taifa na kuungana na mataifa mengine duniani katika maadhimisho hayo.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Soko la Tabata Muslim Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa shirika hilo, Jane Magigita amesema kwa sasa EfG inaendesha mradi unaoitwa "MPE RIZIKI SI MATUSI" ambao umeongeza wigo wa mapambano ya ukatili wa kijinsia  katika Wilaya ya Ilala na Temeke katika masoko sita.

Ameyataja masoko hayo kuwa ni Mchikichini, Kisutu,Tabata Muslim, Feri, Gezaulole na Temeke Stereo.

Magigita aliongeza kuwa, lengo la mradi huo ni kuona wanawake wafanyabiashara wa Manispaa ya Ilala na Temeke wanafanyabiashara katika mazingira huru dhidi ya ukatili wa kingono, kimwili, matusi na kisiasa, vilevile kuona wanawake wakipewa heshima kama binadamu wengine ili waweze kujipatia kipato chao bila vikwazo.

"Mbali na kuwepo mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya ukatili wa kijinsia, EfG pekee ndiyo ambayo inajihusisha na kuwasaidia wafanyabiashara katika masoko na kuwapa elimu ya haki za binadamu, sheria na ukatili wa kijinsia," alisema mkurugenzi huyo na kuongeza;

"Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani tulivyoweza kutambua kuwa sekta isiyo rasmi inasahaulika ukilinganisha na sekta zingine."

Aidha, Magigita alitumia fursa hiyo kulishukuru Shirika la UN Trust Fund kwa kuwawezesha ili kufikia azma mahususi.

Mkurugenzi huyo wa EfG amesema madhumuni ya kuwepo kwetu hapa leo ni kutokana na azma yetu sote kama taifa na kuungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku 16 za kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na pia kuweka msisitizo kwenye utawala wa sheria na upatikanaji wa haki.

"Kama wote tunavyofahamu, chanzo cha maadhimisho haya ni mauaji ya kikatili ya wasichana wa Mirabelle huko nchini Dominika yaliyofanyika mnamo miaka  ya 1960. 
Kutokana na hali hiyo, mwaka 1991, Umoja wa Mataifa ulitenga siku 16 kuanzia Novemba 25 kila mwaka kama siku ya kimataifa ya kuopinga unyanyasaji dhidi ya wanawake. Vilevile, siku ya kuhitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambayo ni Desemba 10," alisema.

Ameongeza kuwa, utafiti unaonyesha wanawake wa Dar es Salaam walio katika sekta isiyo rasmi ndiyo kundi ambalo linakumbwa kwa kiasi kikubwa na ukatili wa kijinsia wawapo nyumbani hata wanapokuwa maeneo yao ya kazi.

Pia utafiti unaonyesha wanawake hao, wanakosa ulinzi toka kwa serikali na mamlaka husika.

"Wanawake wafanyabiashara sokoni ni kundi mojawapo la wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi walioamua kukataa umaskini na kuingia katika harakati za kuinua uchumi wao na familia zao. 

Utafiti uliofanywa na shirika letu la EfG mwaka 2015 ulionyesha kuwa wanawake katika masoko yetu wanafanyakazi kwenye mazingira magumu na wengi wao wakiendesha biashara duni na zenye ufanisi mdogo.

Akisoma risala hiyo kwa mgeni rasmi, Shanisudin Ahmed ambaye ni Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa Segerea aliyemwakilisha Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mheshimiwa Bona Kilua ambaye hakufika kutokana na tatizo la kiafya, Magigita alisema;

" Katika masoko kumi yaliyotembelewa  wakati wa utafiti huu uliofanywa kwenye Manispaa ya Ilala na Temeke ulionyesha kuwa asilimia 95.97% ya wanawake wanapitia ukatili wa kijinsia wanapokuwa mahala pa kazi yaani sokoni, wanawake hawa hukosa mitaji ya kutosha wakati wa kuanzisha baishara, wengi hawana elimu ya usimamizi wa biashara na wala hawashiriki katika kufanya maamuzi na kugombea nafasi za uongozi katika masoko pia ilionekana kwamba hawana dhamana kwa ajili ya kuchukua mikopo, hivyo kubaki na zana na vitendea kazi duni vya kuendesha biashara zao," alisema na kuongeza;

"Ukatili ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara katika masoko ni pamoja na kushikwa maongo ya mwili, lugha chafu na matusi, vitisho, jaribio la kubakwa na kejeli, rushwa ya ngono. Pia utafiti ulionyesha madhara wanayoyapata wanawake hawa katika masoko ambayo ni kushindwa kuzalisha ipasavyo, kuharibika kisaikolojia, kutojiamini, kuwa na hofu, uwoga, kutoheshimika pia kudhalilika," alisema.

Magigita alisema kuwa kupitia mradi wa "MPE RIZIKI SI MATUSI" unaofadhiliwa na Un Trust Fund, shirika limefanikisha kuwafikia wafanyabiashara wapatao 10,250 kwa kuwapa elimu ya ukatili wa kijinsia, sheria na haki za binadamu, kutoa msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia wapatao 1800 ambao mashauri yao yametatuliwa, kutoa rufaa zipatazo 75, masoko 10 yameridhia kuanza kutumia mwongozo wa kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko, kugawa machapisho yapatayo 5,500 kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika kuongeza uelewa wao.

Ameongeza kuwa, wafanyabiashara wameweza kujitambua na wanajua wapi waende kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili, pia kumekuwepo na ongezeko la utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa viongozi wa masoko na polisi, maofisa 120 wa vyombo vya ulinzi na usalama wameongeza uelewa juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, sheria na haki za wanawake jambo lililofanya ukatili masokoni kupungua kwa asilimia 81 kwa mujibu wa utafiti wa Machi 2017 hasa lugha ya matusi na bughudha kwa wanawake.

Mkurugenzi huyo amesema, kupitia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema; "FUNGUKA! UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO HAUMUACHI MTU SALAMA. CHUKUA HATUA" tunakusudia kutoa elimu kwa wafanyabiashara katika masoko yote ili wasikae kimya wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia kwani madhara yake ni makubwa sana na yanarudisha nyuma maendeleo ya taifa letu.

"Ombi letu kwa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya zinazohusika katika kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia ni kuwepo mikakati ya wazi kuhakikisha wanawake katika sekta hii wanapewa kipaumbele ili kuwaweka huru na bughudha zote za ukatili dhidi yao. 

Pia ni muhimu kwa vyombo vya utoaji haki vihakikishe kuwa wanawake wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanapata haki na wale wanaohusika katika kutenda vitendo hivyo wanakumbana na mkono wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine.

"Kwa hili tunaomba jeshi la polisi lishirikiane kwa ukaribu na watoa huduma wetu ambao hutoa huduma ya rufaa kwa wahanga na wapate fursa za kuongeza kipato na kunia uchumi wa taifa," alisema Magigita.

Naye Ahmed aliyemwakilisha Mbunge wa Segerea akizungumza baada ya kusikia risala hiyo alisema amefarijika sana kuona kuwa ili kuinua uchumi na kutokomeza ukatili wa kijinsia si tu kwa wananchi bali kila mtaalam anachukua nafasi yake ili kutoa mchango wake.

"Hili limenipa faraja kubwa mimi binafsi na serikali kwa ujumla hasa hasa katika kuimalishaaa sekta binafsi, mmeweza kuonyesha kwamba kila Mtanzania anafanya bidii kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu katika ukuaji wa sekta isiyo rasmi Tanzania ambayo ipo katika sekta binafsi. Nawashukuru sana EfG kwa kuwa mfano mzuri kwa hili," alisema Ahmed.


Katibu huyo wa Mbunge wa Segerea aliongeza kuwa, Dira ya Taifa inaeleza kuwa Tanzania itakuwa na jamii yenye usawa wa kijinsia ifikapo mwaka 2020. Hatuwezi kufikia dira hiyo tutaruhusu aina ya ukatili wa kijinsia kujitokeza tena au aina mpya kabisa kujitokeza na kukua miongoni mwetu. Tunahitaji kuwa na jamii yenye usawa kijinsia nyakati zote.

"Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kwa hatua hiyo kubwa ya kupeleka huduma hizo kwa wafanyabiashara kwani mara nyingi baadhi ya wafanyabiashara hawafikiwi katika maeneo yao ya biashara na hivyo kukosa fursa ya kukosa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia," alisema Ahmed.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »