RC MGHWIRA-TUMIENI FURSA ZA UTALII KUONDOKANA NA UMASIKINI,WATANZANIA WASHAURIWA

November 30, 2017
Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
WATANZANIA wametakiwa kuzitumia fursa zilizopo kwenye sekta  ya utalii ili kukuza kuongeza vipato na uchumi badala ya kuendelea kulalamika hali ngumu ya maisha.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira amesema wakati wa hafla ya kuwasindikiza mabalozi 9 wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali ulimwenguni wakiwemo na maafisa wa Bodi ya Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje wakati wakipanda mlima Kilimanjaro mkoani hapa jana.
“Hatuna sababu ya kulalamika uchumi, utalii pekee laiti  tungeutangaza vizuri tutafika mbali. Sisi Watanzania hatuoni uzuri tulionao ukienda nchi nyingine ndio utaona, nashauri watu wengi zaidi wapande mlima huu tuliopewa bure na Mungu ili kuona uzuri uliokuwepo,” alisema Bi. Mghwira.
Akizungumza na mabalozi hao aliwashauri wakati mwingine wakifanya shughuli kubwa kama hiyo waje nchini na raia katika mataifa wanayowakisha ili kuongeza tija ya kujitangaza kimataifa.
“Leo wanapanda mabalozi wachache, lakini kama wangekuja na raia mbalimbali kutoka nchi wanazotuwakilisha tungeona zaidi ya watu 80 wanapanda mlima huu na ujumbe ungesambaa zaidi, hivyo nashauri tutumie nafasi hizi kujitangaza vizuri,” alisema Bi. Mghwira.
Aidha, alishauri watu wanaoishia katikati ya safari bila kufika kileleni wapewe vyeti kulingana na maeneo waliyofika kwa sababu kufika tu katika mlima huo ni historia tosha si lazima kufika kileleni ndipo upewe cheti cha utambulisho.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Bi Devota Mdachi alisema wameandaa kazi hiyo ya mabalozi kupanda mlima kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Bank M lengo ni kuonyesha fursa za utalii zilizopo nchini.
“Leo Novemba 29, 2017 mabalozi wanaanza kupanda hadi Disemba 4 ndio tunamaliza, wakifika kileleni watatumia fursa ya kupiga picha na kuweka kwenye mitandao ya kijamii kuitangazia dunia kuwa mlima upo Tanzania lakini pia watahamasisha mabalozi wenzao katika mataifa waliyotoka pamoja na wananchi,” alisema Bi. Mdachi.
Aliongeza kuwa hiyo ni miongoni mwa njia wanayoitumia kutangaza utalii kwa sababu mabalozi wanakutana na watu wengi pamoja na kuhamasisha raia wa nchi wanazotoka kuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini.
Hata hivyo, akizungumzia namna utalii wa ndani Bi. Mdachi alisema: “Watanzania hawatembelei vivutio kwa kutofahamu kwamba kuna viinglio vilivyo chini kwa ajili yao, TTB kazi yetu ni kuhamasisha kwa kutoa taarifa, tumeshirikiana na mamlaka mbalmbal za utalii na sasa watalii wa ndani wanatembelea vivutio yetu.”
Balozi Azizi Mlima kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ambaye pia aliwahi kuwa Balozi nchini Malaysia, alisema mwaka 2014 alishiriki kupanda mlima huo wakiwa mabalozi 18 kwa lengo la kutangaza utalii wa mlima huo kimataifa, ameamua kurudi tena ili kuonyesha heshima yake kwa mlima huo wenye sifa ulimwenguni.
“Tulipopanda mwaka 2014 kati ya mabalozi 18 tuliofika kileleni ni mabalozi 14, mwaka huu tumerejea tena kwa lengo la kuutangaza mlima lakini pia kuhifadhi mazingira. Tunafahamu theluji iliyo kileleni inaanza kuyeyuka na ndiyo maana jana tulianza kwa kupanda miti ili kutunza mazingira,” alisema Balozi Mlima.
Naye Balozi Hemedi Mgaza anayeiwakilisha Tanzania nchini Saudi Arabia amesema wakiwa katika balozi mbalimbali nje ya nchi huwa wanapata maswali mengi kuhusiana na vivutio vya utalii nchini, hivyo anaamini raia wa Saudi Arabia wakimuona amefika kileleni nao watahamasika.
Mwaka huu wanapanda mabalozi 13 wakiwemo maafisa kutoka Bodi ya utalii na Wizara ya mambo ya Nje kwa lengo la kutangaza utalii wa ndani lakini pia kutunza mazingira ya mlima huo, kaulimbiu ya mwaka huu ni Upandaji Mlima Kilimanjaro Diplomasia na Utalii kufikisha katika kilele cha Afrika.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »