RAIS KARIA AWAPA POLE SILABU

November 01, 2017
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametuma salamu za pole kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Athuman Kambi kufuatia ajali ya gari iliyopata timu ya Silabu ya Mtwara.
Gari iliyowabeba wachezaji wa Silabu – mabingwa wa Mkoa wa Mtwara ilipata ajali maeneo ya Mchinga mkoani Lindi wakiwa safarini kwenda Pwani kucheza na Kisarawe United katika mchezo wa awali wa kuwania Kombe la Shirikisho la Azam.
Hakuna aliyefariki, lakini majeruhi 12 wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi.
Mchezo huo ulipangwa ufanyike kesho Alhamisi Novemba 2, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi, mkoani Pwani, lakini umeahirishwa hadi hapo utakapotangazwa tarehe mpya.
Rais Karia amesema kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi hao kupona haraka ili kurejea kwenye majukumu yao ya kawaida hususani mpira wa miguu.
“Mungu awafanyie wepesi,” amesema Rais Karia.
Wakati TFF ikiendelea kusubiri taarifa nyingine, taarifa za awali zinasema msafara ulikuwa na wachezaji 18, benchi la ufundi watano na viongozi watatu. Kulikuwa na taratibu za kuhamisha majeruhi katika Hospitali ya Nyangao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »