TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA

October 19, 2017
LIGI KUU BARA USHINDANI KILA KONA

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea kesho Ijumaa Oktoba 20, 2017 kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu za Mwadui na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga.

Timu hizo zinakutana katika Raundi ya Saba katika duru hili la kwanza la VPL ambalo mbali ya Kampuni ya Simu ya Vodacom - wadhamini wakuu, wadhamini wengine ni Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) na Benki ya KCB ambayo huduma zake za kibenki zinazidi kushamiri nchini.

Wadhamini hao wanachagiza ligi hiyo ambayo itaendelea Jumamosi Oktoba 21 kwa michezo sita  itakayofanyika kwenye viwanja tofauti huku mechi nyingi zikipata fursa ya kuonyeshwa kwenye chaneli mbalimbali za Azam Tv kupitia king’amuzi cha Azam.

Michezo ya Jumamosi itakutanisha timu za Mbao na Azam kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati Lipuli itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa ilihali Ruvu Shooting watakuwa wageni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumamosi hiyo hiyo Simba yenye mabadiliko kidogo kwenye benchi la Ufundi, itawaalika Njombe Mji kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Ndanda ikicheza na Singida United kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wakati Jumamosi hiyohiyo tena, Mtibwa Sugar wakicheza na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu - ambao ni kati ya Stand United na mabingwa watetezi, Young Africans ya Dar es Salaam - mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.



LIGI DARAJA LA KWANZA KUENDELEA WIKIENDI HII

Raundi ya Sita ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaendelea  kesho Ijumaa Oktoba 20, 2017 kwa mechi za makundi yote matatu.

Katika Kundi ‘A’, Mvuvumwa FC ya Kigoma, watacheza na Mgambo JKT katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mvuvumwa anatumia Kanuni ya 6 (1) na (2) kuhamishia mechi zake za nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kutoka Uwanja wa Tanganyika, Kigoma.

Mechi nyingine kwenye kundi hilo itafanyika Jumapili Oktoba 22, mwaka huu kwa michezo mitatu.

Mechi hizo ni kati ya  Kiluvya United  na Mshikamano  kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, ilihali African Lyon  itacheza na Ashanti United  kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Friends Rangers itapambana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam, Dar es Salaam.

Katika Kundi ‘B’ siku hiyo ya Ijumaa Oktoba 20, mwaka huu Polisi Dar itacheza na Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam wakati michezo mingine katika kundi hilo ikichezwa Jumamosi na  Jumapili.

Jumamosi Mbeya Kwanza itacheza na JKT Mlale Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani na Jumapili Polisi Tanzania watawakaribisha KMC kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika Moshi, huku Mawenzi Market ya Morogoro wakiwaalika Mufindi United kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Katika Kundi ‘C’ kutakuwa na mchezo mmoja siku ya Ijumaa Oktoba 20, 2017 Pamba SC ya Mwanza itacheza na Alliance Schools nayo ya Mwanza kwenye Uwanja wa Nyamagana huko Mwanza na michezo mingine itafanyika Jumamosi na Jumapili.

Michezo ya Jumamosi  itazikutanisha Biashara Mara dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Karume Mara,Transit Camp itakuwa mwenyeji wa Dodoma FC kwenye Uwanja wa Kambarage Mjini Shinyanga,wakati mchezo mwingine wa Kundi C, Toto Africans ya Mwanza itacheza  na Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »