Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitoa hundi ya Mkopo uliotolewa na SIDO
kwa mjasiriamali Sarah Isaya kutoka Singida katika hafla fupi ya kukabidhi
mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani hapa.
Mkurugenzi
Mtendaji SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji akitoa nasaha zake
kwenye hafla ya utoaji wa hundi za mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani
Singida uliofanyika kwenye viwanja vya SIDO mjini hapa. Wa kwanza kushoto
(aliyekaa) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitazama ubora wa mafuta ya alizeti na kupata maelezo ya mafuta hayo yanayosindikwa
katika viwanda vya Mkoa wa Singida kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya
kuzalishaji Mafuta ya alizeti ya Sunshiwe Oil Mill, Salum
Khalifan.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amelitaka shirika la Viwanda Vidogo
vidogo (SIDO) kuandaa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo mbali mbali
mkoani hapa ili wakihitimu waweze kujiajiri
Dkt.
Nchimbi ametoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mikopo
ya SIDO kwa wajasiriamali iliyofanyika kwenye viwanja vya SIDO ambapo amesema
mafunzo hayo yatawajengea mazingira mazuri wahitimu kujiajiri.
Amesema
Mkoa wa Singida una fursa nyingi za kujiajiri pamoja na kuwa na vijana wengi
hasa walipo katika vyuo mbalimbali lakini hawawekezi katika fursa hizo kwa kutokujua
au kukosa elimu ya kutosha juu ya ujasiriamali, na hata waliopo vyuoni
wakihitimu wanasubiri kuajiriwa badala ya kujiajiri.
Dkt.
Nchimbi amesema ili wananchi wakiwemo vijana waweze kuzitambua fursa hizo, SIDO
Mkoa na wadau wengine wanapaswa kuongeza juhudi zaidi katika utoaji mafunzo ya
ujasiriamali ambapo amewataka wajielekeze kwenye vyuo mbalimbali.
“Singida
ina kila aina ya fursa ambazo zinaweza kumkomboa mwananchi kiuchumi. Kwa hiyo
hakuna sababu vijana au watu wengine kuukimbia mkoa wao na kwenda kutafuta
maisha katika mikoa mingine. Ni suala la kujipanga na kupata fursa ya mafunzo
kutoka SIDO mkoa”, amefafanua.
Aidha
ameziagiza halmashauri zote na manispaa Mkoani hapa kutangaza fursa, bidhaa,
mazao, na huduma zinazopatikana katika maeneo yao ili kuwasaidia wajasiriamali
kupata soko la uhakika.
“
Halmashauri zote tumieni fedha mnazopata kwenye vyanzo vya mapato ya ndani muwasaidie wajasiriamali wenu kutangaza
kwenye vyombo vya habari, nina imani na uhakika kuwa mkitangaza bidhaa na mazao
yao yatapata soko na nyinyi halmashauri mtapata mapato yenu”, amesema
Dk.Nchimbi.
Awali
Mkurugenzi Mtendaji wa SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji amesema
SIDO imekuwa tegemeo kubwa kwa wajasiriamali hasa katika kutoa mafunzo na
kusaidia teknolojia ya kuongeza thamani ya mazao na malighafi.
“Mikopo
ya SIDO imeweza kuwasaidia wajasiriamali kuthubutu na kuanzisha miradi ya
usindikaji mara tu baada ya kupata mafunzo. Kundi hili limekuwa na changamoto
ya mitaji kwa kuwa halikidhi na halijaweza kuthubutu kuzifikia benki kutokana
na woga na gharama za mikopo”, amesema.
Mhandisi
Profesa Mpanduji amesema kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 SIDO imeweza kutoa
mikopo 4,464 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.2. Mikopo hiyo
imetengeneza ajira 11,861 kati ya ajira hizo asilimia 51 ni wanawake.
Kwa
upande wake Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende amesema kwa Mkoa wa
Singida wametoa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 724.6 kwa wajasiriamali
693 na vikundi 47. Hali ya urejeshaji wa mikopo hiyo ni asilimia 98.
Kibende
amesema SIDO wameweza kutoa mafunzo ya wajasiriamali mbalimbali 37 kwa
wajasiriamali 996 ambao kati yao wanawake walikuwa 536 na wanaume 460.
Amesema
baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa wafanyakazi na ukosefu
wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango waliyojiwekea ikiwemo kuendeleza na
kuboresha mtaa wa viwanda.
Naye
Mjasiriamali kutoka Kampuni ya Singida Super Quality Oil and Rice mills Simon
Kitundu amezishauri halmashauri na manispaa kutenga maeneo maalum ya kufanyia
biashara wajasiriamali waweze kuondokana na adha mbalimbali ikiwemo ya kuuza
bidhaa zao kwenye madirisha ya mabasi.
EmoticonEmoticon