Sehemu
ya Bonde la Manonga mkoani Tabora ambalo miamba yake inaonesha
uwezekano wa kuwa na viashiria vya Mafuta kutokana na sifa zake za
Kijiolojia na Kijiofizikia.
Timu
ya wataalam kutoka Uganda na Tanzania wakiwa katika miamba inayoonekana
katika kijiji cha Mwanzugi wilayani Igunga ikiwa ni ikiwa ni maandalizi
ya shughuli za Utafiti wa Mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere na Ziwa
Tanganyika.
Timu
ya wataalam kutoka Uganda na Tanzania wakiwa katika Bonde la Manonga
lililopo katika kijiji cha Kining’inila mkoani Tabora ambapo pia
walichukua sampuli za miamba katika Bonde hilo ikiwa ni maandalizi ya
shughuli za Utafiti wa Mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere na Ziwa
Tanganyika. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na
Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo.
Timu
ya wataalam kutoka Uganda na Tanzania wakiwa katika eneo la Sekenke
mkoani Singida ambapo miamba ya Bonde la Wembere inaonekana ikiwa ni
maandalizi ya shughuli za Utafiti wa Mafuta katika Bonde la Eyasi
Wembere. Wa Tano kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Maendeleo ya Madini (Uganda), Robert Kasande, wa Pili kushoto ni Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania), Dkt Mhandisi
Juliana Pallangyo na wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Nishati,
Mhandisi Innocent Luoga.
Na Teresia Mhagama, Tabora
Imeelezwa
kuwa miamba iliyo katika Bonde la Eyasi Wembere hususan mabonde madogo
(sub basin) ya Wembere na Manonga yaliyopo katika mikoa ya Tabora,
Shinyanga, Singida na Simiyu inawezekana kuwa na mafuta kutokana na sifa
zake za Kijiolojia na Kijiofizikia.
Hayo
yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya
Madini (Uganda), Robert Kasande na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati
na Madini (Tanzania), Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo katika Mkutano na
Wananchi uliofanyika katika kijiji cha Mwashiku wilayani Igunga mkoani
Tabora. Mkutano huo uliandaliwa na Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey
Mwanry.
Viongozi
hao walitoa kauli hiyo baada ya timu ya wataalam kutoka Uganda na
Tanzania kufanya ziara katika Bonde hilo hususan mabonde madogo ya
Wembere na Manonga na kutembelea miamba inayoonekana katika maeneo ya
Sekenke mkoani Singida, na vijiji vya Mwanzugi na Kining'inila mkoani
Tabora.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya
Madini wa Uganda alieleza kuwa baada ya kuona dalili hizo Timu hiyo
itatoa mapendekezo mbalimbali kwa Wataalam wa Tanzania ili kuweza
kufikia lengo la Serikali la kuchimba Mafuta katika Bonde la Eyasi na
Ziwa Tanganyika .
Alisema
kuwa endapo Mafuta yatapatikana katika Bonde hilo yataweza kusafirishwa
katika Bomba la Mafuta linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya
Tanga na kuweza kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza
kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa Tanzania kugundua mafuta katika Bonde
hilo kwani nchini nyingine ambazo Bonde hilo linapita kama Kenya na
Uganda tayari wamegundua Mafuta.
Naibu
Katibu Mkuu, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo alisema kuwa kupatikana
kwa mafuta katika eneo hilo kutaimarisha hali ya uchumi nchini na
kuwaasa wananchi kujiandaa na fursa za kiuchumi ikiwemo utoaji wa huduma
mbalimbali wakati wataalam wakiwa wanafanya shughuli mbalimbali za
kitafiti katika eneo husika.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry aliwataka wananchi
wanaozunguka Bonde hilo na Viongozi wa Serikali katika Mkoa huo kutoa
ushirikiano kwa wataalam watakaofanya kazi za kitafiti ili zoezi hilo
liweze kufanyika kwa ufanisi.
Naye,
Mjiofizikia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli, (TPDC), Sindi
Maduhu alisema kuwa bonde hilo la Eyasi Wembere lina ukubwa wa Kilomita
za mraba 19,197 likiwa na takwimu za awali za kijiofizikia (Airborne
gravity gradiometry) zilizokusanywa na kutafsiriwa mwaka 2015/2016.
EmoticonEmoticon