Kocha Mkuu wa timu za vijana Tanzania, Kim Paulsen, amevutiwa na
uwezo wa vijana wanaoibuka kila mwaka katika soka nchini na kusema tuna
hazina ya wachezaji wenye uwezo wa kucheza mahala popote duniani.
Poulsen amewaambia waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 26, 2017
jijini Dar es Salaam kwamba wamefanikiwa kuona uwezo wa vijana kwa
wakati wote, lakini umahiri umekuwa ukiongezeka kwa kila timu mpya
inapoitwa.
Kwa takribani mwezi mmoja, Kocha Poulsen akishirikiana na Oscar Mirambo walikuwa kwenye programu ya kuinoa Serengeti Boys mpya.
“Hii Serengeti mpya inayokuja, nayo ni bora kama ilivyo kwa wale
waliopita. Bado naona kuna vipaji vikubwa sana. Ni kulea tu hawa vijana
kazi ambayo tutaendelea nayo.”
Poulsen - Raia wa Denmark amesema kambi ya vijana 57 walioripoti na
kufundishwa na makocha hao, wameonesha uwezo mkubwa, lakini kiufundi
wamepunguza hadi hadi kubaki 27.
Amesema hao waliobaki watapangiwa kambi nyingine itakayoanza Novemba
19, 2017 na itafikia mwisho Desemba 19, mwaka huu baada ya kuivunja
kambi ya muda jana Septemba 25, mwaka huu.
Katika programu ya kambi hiyo mpya ya Novemba na Desemba, Kocha Kim
ametaka angalau mechi moja ya kirafiki ya kimataifa huku akisisitiza
apate timu ya nchi iliyowekeza hasa katika soka la vijana: “Ikiwezekana
hata mbili.”
Akizungumzia kuhusu ujio mpya wa timu ya taifa ya Vijana wenye umri
wa chini ya miaka 20 - Ngorongoro Heroes, Kocha Kim amesema itaitwa
kambini wakati wowote kuanzia Oktoba mwanzoni kwa kambi ya wiki tatu.
“Timu ya Serengeti Boys iliyopita ilifanya vizuri sana. Ni matarajio
yetu hata hii itafanya vizuri, lakini hapa nataka nizungumzie ile
iliyoshiriki fainali za AFCON u17 nchini Gabon…
“…kwa hiyo kambi itakayoitwa ya Ngorongoro Heroes, tutaita wale wote
waliounda Serengeti Boys iliyopita. Hata wale ambao hawakubahatika
kwenda Gabon tutawajumuisha kwa ajili ya kambi ya wiki tatu mwezi
Oktoba,” amesema Poulsen.
Amesema kwamba sababu za kuita nyota wale wa Serengeti Boys katika
Ngorongoro Heroes ni kuwapa nafasi ya kwanza wao kuonekana kama wangali
na uwezo wa kupambana kama ilivyokuwa zamani na kwa wale wenye uwezo tu,
ndio watakaochukuliwa,” amesisitiza.
EmoticonEmoticon