Mwezeshaji wa mafunzo ya nembo na vifungashio, Emmanuel Bakashaya,
akifundisha akinamama wa Green Voices jinsi nembo na vifungashio vinavyopaswa
kuonekana.
Akinamama wa Green Voices wakiwa katika ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
wakijifunza kutoka kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Raymond Wigenge, hivi
karibuni.
Green Voices katika majadiliano ya vikundi juu ya njia mbali
mbali za kutafuta rasilimali wakati wa mafunzo chini ya mwezeshaji Richard
Jackson.
Green Voices wakiangalia bidhaa za ujasiriamali za Mama
Rocky (mwenye mtandio wa buluu) katika supermarket. Hii ni baada ya kumtembelea
kiwandani kwake katika ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda
Vidogo (SIDO) jijini Dar es Salaam.
Dkt. Alicia Cedaba, Meneja wa Mradi wa Green Voices kutoka
Hispania, akifundisha akinamama wanaotekeleza mradi huo nchini Tanzania.
Akinamama wa Green Voices wakiwa katika mafunzo kwa vitendo
katika makao makuu ya SIDO jijini Dar es Salaam.
Green Voices baada ya kuhitimu mafunzo. Walioketi kutoka
kushoto ni Mratibu wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya,
Mkurugenzi wa taasisi ya IMED iliyotoa mafunzo, Dkt. Donath Olomi na Meneja wa
Mradi wa Green Voices kutoka Madrid, Hispania, Dkt. Alicia Cebada.
AKINAMAMA
wanaotekeleza mradi wa Green Voices nchini Tanzania sasa wanalenga kuboresha
bidhaa za kilimo wanazozalisha ili kuongeza tija ikiwa ni katika azma yao ya kupambana
na mabadiliko ya tabianchi.
Wakizungumza
baada ya semina ya wiki moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni,
akinamama hao walisema elimu waliyoipata imewapa mwanga wa kuendeleza miradi
yao na kuhakikisha wanaboresha bidhaa zao ili ziwezi kuingia katika soko la
ushindani.
Miradi
inayotekelezwa kupitia Green Voices Tanzania ni kilimo cha mihogo, kilimo cha
matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki, ukaushaji wa mbogamboga na utengenezaji wa
majiko rafiki wa mazingira ambayo inatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam,
Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro.
“Nilikuwa
nimekata tamaa nisijue nitauendelezaje mradi wangu, lakini kwa mafunzo
niliyoyapata kutoka kwa wataalam mbalimbali, hakika nimehamasika na kuona
kwamba ninaweza kusimama na kusonga mbele,” alisema Farida Makame ambaye
anasimamia mradi wa Majiko
ya Umeme-Jua mkoani Kilimanjaro.
Farida
alisema amehamasishwa zaidi na mafunzo hayo, ambayo yamempatia mbinu mpya zaidi
za kuendeleza mradi huo kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa
upande wake, Abiah Magembe anayesimamia mradi wa Usindikaji
wa Muhogo na Mtama katika Kijiji cha Kitanga, Wilaya ya Kisarawe mkoani
Pwani, amesema mafunzo ya jinsi ya kufungasha na kuweka nembo kwenye bidhaa
yamempa mwanga mkubwa na kwamba sasa yeye na wenzake watazalisha bidhaa zao kwa
kujiamini na kuziingiza kwenye soko la ndani na la kimataifa.
“Tunatengeneza
bidhaa nyingi zinazotokana na muhogo na zina viwango vizuri, lakini kwa mafunzo
tuliyoyapata, sasa tunaweza kuziboresha kwa kuhusisha taasisi husika kama Shirika
la Taifa la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ili tuingie
kwenye ushindani wa kitaifa na kimataifa,” alisema Bi. Magembe.
Bi.
Magembe alisema kwamba, bidhaa wanazozalisha kutokana na zao la muhogo ni unga
unaotumika kwa uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, skonzi, biskuiti,
mandazi, sabuni ya unga pamoja na bidhaa nyingine nyingi.
Mazao
mengine yanayopatikana katika muhogo ni mzizi wenyewe ambao unatafunwa mbichi
au ukiwa umepikwa au kukaangwa, kwenye futari, miti na majani huweza kuzalisha
bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi, mafuta, kilevi, dawa
za binadamu na plastiki wakati ambapo wanga (starch) hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani,
rangi za awali za ukuta na sukari (sugar
syrup).
Takwimu
za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani
kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalisha takriban tani milioni 102.6 kila
mwaka.
Tanzania
ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya
Nigeria, Ghana na Congo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za
ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia
15 za chakula kwa nchi nzima na karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Regina
Kamuli ambaye anasimamia mradi wa Majiko
Banifu wilayani Mkuranga, alisema anashukuru wanakikundi wenzake
wamejizatiti na sasa wanapata fursa ya kushiriki katika maonyesho mbalimbali
yakiwemo ya kilimo kuonyesha majiko hayo ambayo ni rafiki wa mazingira.
“Hivi
sasa baada ya kikundi kusajiliwa akinamama wamenufaika na mikopo nafuu kutoka
Halmashauri ya Wilaya na kwa mafunzo haya tutaboresha majiko yetu ili tuyanadi
katika maeneo mengi nchini Tanzania kwa sababu yanatumia kuni kidogo, hivyo
kuokoa mazingira,” alisema Regina.
Magdalena
Bukuku anaongoza kikundi cha akinamama wanaoshiriki Kilimo
cha Uyoga huko Bunju jijini Dar es Salaam, ambapo anasema mafunzo ya
ufungashaji na uwekaji wa nembo yamempa mwanga mkubwa ili kwenda kuboresha
bidhaa zao ziingie kwenye ushindani.
“Tunazalisha
uyoga kwa wingi kwa sasa na wateja wameongezeka, hata hivyo, ikiwa tutafungasha
vizuri na kupanua kilimo chetu tunaweza kulifikia hata soko la kimataifa,”
alisema.
Mariam Bigambo na Monica Kagya wao wanashiriki
ufugaji wa nyuki ambapo mbali ya kuvuna asali, lakini wanasaidia kutunza
mazingira na kuongeza tija katika mazao ya kilimo kutokana na uchavushaji.
Wakati
Mama Bigambo anaendesha Ufugaji
wa Nyuki huko Dakawa, Morogoro, Bi. Monica yeye na akinamama wenzake wana
jukumu kubwa la kutunza misitu ya Pugu na Kazimzumbwi wilayani Kisarawe
kutokana na Ufugaji
wa Nyuki.
“Tunataka
tujikite katika kufungasha vizuri asali na kuziwekea nembo ili tuingie kwenye
ushindani,” walisema.
Suala la ufungashaji na uwekaji wa nembo nalo limewagusa Esther
Muffui, Dkt. Sophia Mlote na Leocadia Vedasto ambao wanashiriki katika kilimo
na ukaushaji wa mboga na matunda.
“Tunajihusisha
na Ukaushaji
wa Mboga na Matunda kule Morogoro, sasa tulikuwa tunashindwa kufungasha
vizuri, naamini tumepata mwanga wa namna ya kufungasha bidhaa zetu ili tupate tija
zaidi,” alisema Bi. Esther.
Leocadia
yeye anashiriki mradi wa Kilimo
na Usindikaji wa Viazi Lishe huko Ukerewe mkoani Mwanza wakati Dkt. Mlote anashiriki
mradi wa Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga Kinyerezi
jijini Dar es Salaam.
Naye Evelyn
Kahembe ambaye anaendesha Kilimo cha Matunda huko Uvinza, Kigoma, amesema
mafunzo hayo yamemuongezea ujasiri wa kuendeleza mradi huo akishirikiana na
wanawake wengine huko Kigoma.
Kwa
upande wake, Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya,
alisema mafunzo waliyoyapata yametoa mwanga mkubwa kwa washiriki na kuleta
mtazamo wa kibiashara zaidi tofauti na hapo mwanzo.
“Suala
la ufungashaji wa bidhaa ni la muhimu na imekuwa vyema tumepata mafunzo ya kina
pamoja na kutembelea taasisi kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na
Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), tumejifunza mengi ambayo
yamebadili mtazamo wetu,” alisema Secelela.
EmoticonEmoticon