MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, POLE SIMBA SC
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma
salamu rambirambi kwa Rais wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Evans
Aveva kutokana kifo cha shabiki wa timu hiyo, Shose Fedeline aliyefariki
dunia jana mchana Mei 28, 2017 katika ajali ya gari.
Kadhalika,
Rais Malinzi ametuma salamu za pole kwa majeruhi katika ajali hiyo
akiwamo Nahodha wa Simba, Jonas Mkude na dereva wa gari hilo ambalo
lilikuwa safarini kurejea Dar es Salaam kutoka Dodoma.
Wanafamilia
kadhaa wa mpira wa miguu walikuwa Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita
kushuhudia mchezo wa fainali za Kombe la Azam - ASFC (Azam Sports
Federation Cup HD 2016/17) uliozikutanisha timu za Simba na Mbao FC ya
Mwanza. Mbao ilifungwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa dakika 120.
Gari
lililopata ajali ni aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilianguka na
kuzunguka mara kadhaa na baadaye kutulia katika eneo la Dumila mkoani
Morogoro baada ya tairi yake ya nyuma kupasuka hivyo kumshinda dereva na
kupoteza mwelekeo kutoka barabara kuu.
“Nakuandikia
Rais wa Simba, Bw. Evans Aveva, pia ndugu, jamaa na marafiki pamoja na
majirani wa marehemu Shose Fideline na wanafamilia wengine wa mpira wa
miguu, kwamba nimepokea taarifa za ajali ya gari iliyosababisha kifo cha
mmoja wa mashabiki wa timu ya Simba kwa masikitiko makubwa sana. Wito
wangu, nawaomba wanafamilia wote kuwa watulivu na moyo wa subira katika
kipindi hiki kigumu,” amesema Rais Malinzi.
Msiba
wa shabiki huyo wa Simba umetokea wakati Simba imetawazwa kuwa mabingwa
wapya wa Kombe la Azam likihitimisha ushindani wa timu 86 na hivyo kuwa
na hati ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika
(CAF) hapo mwakani.
Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema, Shabiki wa Simba, Shose Fedeline.
“Pia
nawapa pole nyingi sana majeruhi wote katika ajali hiyo akiwamo Jonas
Mkude ambaye ni Nahodha wa Simba na Nahodha Msaidizi wa Timu ya Tanzania
‘Taifa Stars’. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wapone haraka
ili kujiunga na shughuli zao mbalimbali za ujenzi wa nchi,” amesema
Rais Malinzi.
Kadhalika,
Rais Malinzi ameipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa huo wa ASFC hivyo
pamoja na zawadi nyingine kama vile Sh 50 milioni na medali za ubingwa
pia Simba imepata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Shirikisho -
michuano inayoandaliwa na CAF.
“Naitakia Simba maandalizi mema ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani,” amesema Rais Malinzi.
TAIFA STARS KUWEKA KAMBI MISRI, MKUDE ABAKI
Kikosi cha wachezaji 20 wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti, kinatarajiwa kuondoka kesho Jumanne saa 10.45 jioni kwenda Misri.
Taifa
Stars ambayo itakuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kesho saa 7. 45
mchana inakwenda Misri kufanya kambi ya siku nane kujindaa na mchezo
dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Wachezaji
hao 20 kutoka hapa Tanzania wataungana na na wengine watatu, Nahodha
Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Faridi Mussa wanaocheza ughaibuni
katika kikosi hicho na kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23 nchini Misri.
Nahodha
Msaidizi, Jonas Mkude hatakuwako kwenye msafara huo kutokana na ushauri
wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo wa Simba apate mapumziko ya
angalau siku nne.
Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia na kusema kuwa Mkude
ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri.
Mayanga hajajaza nafasi ya Mkude.
Mchezo
dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa
Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za
Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika
NCHINI Cameroon.
Mbali
ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na
Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa
katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.
Kikosi cha Taifa Stars kinachofundishwa na Kocha Salum Mayanga kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno Kakolanya (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Walinzi
wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan
Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba)
na Haji Mwinyi (Yanga SC).
Walinzi
wa kati Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi
Banda (Simba SC) na Agrey Morris (Azam FC) ilihali viungo wa kuzuia ni
Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na
timu kwa sasa.
Viungo
wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC) na
Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga
SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji
wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC
Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera
Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).
Wasaidizi
wa Mayanga katika benchi la ufundi ni Novatus Fulgence ambaye ni kocha
msaidizi Patrick Mwangata - kocha wa makipa pia yumo Meneja wa timu,
Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu, Daktari wa timu ni Richard Yomba
na Daktari wa viungo ni Gilbert Kigadya.
Timu
hiyo iliingia kambini Machi 23, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar
es Salaam kabla ya kesho kwenda Misri na baadaye itarejea Tanzania
kucheza na Lesotho, Juni 10, mwaka.
MAREKEBISHO YA KANUNI ZA LIGI KUU YA VODACOM NA LIGI DARAJA LA KWANZA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatangazia klabu zote zinazoshiriki
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/18 na zile za Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2017/18 kwamba kipindi hiki ni cha
kuwasilisha maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu marekebisho ya kanuni
za ligi husika.
TFF
inaagiza klabu zote - kwa nafasi walizonazo kama wanafamilia ya mpira
wa miguu, kuwasilisha mapendekezo na maoni kuhusu marekebisho ya katiba
kwa njia ya kuyatuma kupitia anwani za sanduku la Barua 1574, Dar es
Salaam au barua pepe tplb.tplb@yahoo.com au yaletwe moja kwa moja ofisi za Bodi ya Ligi au TFF.
Maoni
hayo tayafanyiwa kazi na Bodi ya Ligi kabla ya kupelekwa kwenye kikao
cha Kamati ya Utendaji kabla ya kuanza msimu husika wa mashindano baada
ya kupita msimu uliopita.
EmoticonEmoticon