Nimesoma na kuona katika vyombo
mbalimbali vya habari kuhusu vurugu zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017
katika hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es salaam, zinazosemekana
kuhusisha wanachama wa CUF.
Ni ukweli usiopingika kuwa, suala
la mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini
nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii
kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa; nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa
hususani wanachama wa chama cha CUF, kutambua kwamba, kuwapo kwa shauri
mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani
jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.
Hivyo, ninalaani vurugu hizo,
ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na
tunu zetu za taifa za amani na utulivu. Pia, nawaasa wanachama wa CUF
pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yapo mahakamani hebu
tuheshimu utawala wa Sheria.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote
yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hivyo,
hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka taratibu za kuendesha
chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.
Aidha, ninaviasa vyama vya siasa
kuelewa kuwa havipo juu ya Sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria
za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu tulionao.
Mwisho, ninaomba vyombo vya ulinzi
na usalama katika nchi yetu kulifanyia kazi tukio hilo, ili wahusika
wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kwa upande wa Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama
vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.
Jaji Francis S.K. Mutungi
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
24 Aprili, 2017
EmoticonEmoticon