RAIS WA BENKI YA DUNIA AONDOKA NCHINI BAADA YA ZIARA YAKE YA KIKAZI YA SIKU TATU

March 21, 2017


Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim, ameondoka nchini baada ya ziara ya kikazi ya siku tatu na kuagwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake ya Siku tatu Dkt. Jim Yong Kim, pamoja na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jonh Pombe Joseph Magufuli, alishiriki tukio la uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya juu (Ubungo Interchange) katika makutano ya barabara Ubungo itakayogharimu Sh.188.7 Bilioni kati ya hizo Benki ya Dunia itatoa Sh186.8 kwa ajili ya ujenzi na usanifu na Sh1.9 Bilioni zitatolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa fidia.

Aidha umma umeshuhudia utiwaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo itakayo fadhiliwa na Benki ya Dunia hapa nchini, yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.74.

Miradi hiyo ni ile ya Uboreshaji Miundombinu ya Usafiri Jijini Dar es Salaam ikiwemo awamu ya tatu na ya nne ya mradi wa mabasi yaendayo haraka-DART, Mradi wa kusambaza maji safi, mazingira na ukusanyaji wa maji taka, na mradi wa uendelezaji wa miji ya Arusha, Dodoma, Tanga, Kigoma, Mwanza, Mbeya, na Mtwara.

Pia katika ziara hiyo, Dkt. Kim alipata fursa ya kutembelea Shule ya Msingi Zanaki iliyopo Manispaa ya Ilala, ambayo ni moja ya Shule zinazonufaika na mpango wa kuboresha elimu ya msingi. 
Rais wa Benki ya Dunia (WB) Dkt. Jim Yong Kim (wa pili) na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kushoto), wakitoka katika eneo la kupumnzikia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Waziri Mpango amemuaga Rais huyo baada ya kuwepo nchini kwa takribani siku tatu.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akiagana na Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim (wa pili kushoto) baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi hapa nchini, ambapo alishiriki uwekaji wa jiwe la Msingi katika ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (aliyevaa tai) akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa kumuaga Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim aliyekuwepo nchi kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kulia) wakiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kumuaga Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim, muda mfupi kabla ndege iliyombeba Rais huyo kuondoka.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto) na afisa mwingine wa Serikali wakishuhudia wakati Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia katika nchi ya Tanzania, Malawi, Somalia na Burundi, Bi. Bella Bird wakibadilishana mawazo baada ya Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim kuondoka nchini. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »