Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Maafisa Mawasiliano Serikalini
wametakiwa kutumia tovuti za ofisi na tovuti kuu ya Serikali kwa kuweka
taarifa mbalimbali zinazohusu huduma na bidhaa zinazotolewa na taasisi
hizo ili kuwawezesha wananchi kuzifahamu huduma hizo kirahisi.
Rai hiyo imetolewa leo Mkoani
Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (EGA), Dkt. Jabir
Bakari alipokuwa akitoa semina juu ya matumizi na umuhimu wa tovuti za
Serikali katika kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano Serikalini
kinachoendelea Mkoani humo.
Dkt. Bakari amesema dhana ya
Serikali Mtandao ni kuhuisha matumizi ya TEHAMA kwenye utoaji wa
taarifa mbalimbali za Serikali kwa wananchi hivyo ni muhimu kwa kila
taasisi kuwa na tovuti zenye taarifa za uhakika na zinazoendana na
wakati ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
“Wakala kwa kushirikiana na
TAMISEMI pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
tumetengeneza mfumo unaotumia muda mfupi kwa taasisi za Serikali
kutengeneza tovuti zao ili ifikapo Juni mwaka huu taasisi zote ziwe na
tovuti zao zitakazowarahisisha wananchi kufahamu huduma
kirahisi,”alisema Dkt.Bakari.
Mtendaji Mkuu huyo ameongeza kuwa
tovuti za taasisi zisitumike tu katika kutoa taarifa za huduma na bidhaa
zao bali zitumike kuelezea mambo mengine muhimu yanayofanywa na taasisi
hizo.
Akielezea kuhusu tovuti kuu ya
Serikali, Dkt. Bakari amesema ni muhimu kuhakikisha taarifa muhimu na
za kudumu za taasisi husika zinawekwa ili kusaidia wananchi kufahamu
kiundani kazi wanazozifanya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Chama cha Maafisa Mawasiliano (TAGCO), Bw.Innocent Mungy amesema mbali
na kuweka taarifa katika tovuti za Serikali, ni wajibu wa Maafisa
Mawasiliano Serikalini kutumia mitandao ya kijamii kufikisha taarifa
muhimu kwa wananchi .
“Kutokana na maendeleo ya
teknolojia duniani hasa katika upande wa mawasiliano, matumizi ya
mitandao ya kijamii yamekuwa yakileta tija kwa taasisi za Umma kwani
yanasaidia Serikali kujibu haraka hoja zinazowasumbua wananchi”alisema
Mungy.
Pia aliwataka Maafisa Mawasiliano
kuwa wabunifu katika kutumia mitandao ya kijamii kwani mitandao hiyo
inatoa fursa ya kushirikiana, kutangaza huduma na bidhaa za taasisi,
kufahamu matatizo ya wananchi.
EmoticonEmoticon